Abbas atembelea Israel
29 Desemba 2021Vyombo vya habari viliripoti kwamba mkutano huo ulifanyika nyumbani kwa Gantz iliyopo katikati ya mji wa Rosh HaAyin.
Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Israel ilisema katika mazungumzo hayo ya Jumanne (28 Disemba), Gantz alimuambia Abbas kwamba anadhamiria "kuendeleza mambo yanayoimarisha kuaminiana kati ya pande hizo mbili katika maeneo ya uchumi na kiraia" kama ambavyo walikubaliana katika mkutano wao wa mwisho.
Siku ya Jumatano (Disemba 29), Waziri wa Masuala ya Kiraia wa Palestina, Hussein al Sheikh, alituma ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter akithibitisha kuwa Rais Abbas alikutana na Gantz.
"Mkutano huo ulihusu umuhimu wa kuandaa jukwaa la kisiasa litakalotupelekea kwenye suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa. Pia wawili hao wamejadiliana hali tete sana iliyopo sasa kutokana na matendo ya walowezi na pia masuala ya kiusalama, kiuchumi na kibinaadamu," aliandika Al-Sheikh.
Bennet, Likud wapinga
Lakini mara tu baada ya mazungumzo hayo, waziri mkuu mwenye siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel, Naftali Bennett, alibainisha kwamba hakukuwa na mchakato wowote wa amani na Wapalestina na kwamba "kamwe hautakuwapo."
Chama cha upinzani kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia nchini Israel, Likud, kililaani mkutano huo, kikisema kwamba uamuzi wa kuridhia mambo ambayo ni hatari kwa usalama wa Israel una siku chache tu kufikiwa.
Likud, ambacho kiliondoshwa madarakani kwenye uchaguzi uliopita chini ya Benjamin Netanyahu, kilirejelea kauli yake dhidi ya serikali ya sasa ya mseto chini ya Naftali, ambayo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Israel inajumuisha chama cha Waisraili wenye asili ya Kiarabu.
"Serikali ya Waisraeli na Wapalestina imewarejesha Wapalestina na Abbas kwenye ajenda... na hilo ni hatari kwa Israel," kilisema chama hicho.
Hamas nayo yapinga mkutano wa Abbas na Gantz
Ukosoaji kama huo umetoka pia Ukanda wa Gaza kutoka kundi linalotawala huko, Hamas, ambalo limesema ziara ya Abbas nchini Israel inakwenda kinyume na moyo ya utaifa wa watu wa Palestina.
"Tabia hii ya uongozi wa Mamlaka ya Palestina inazidisha mpasuko wa kisiasa wa Wapalestina, inaikanganya hali ya Palestina, inawapa nguvu wale wanaotaka kurejesha mahusiano na wakaliaji kimabavu, na inadhoofisha msimamo wa Wapalestina dhidi ya urejeshaji huo wa mahusiano." Alisema msemaji wa Hamas, Hazem Qassem.
Hii ni mara ya pili kwa Abbas na Gantz kukutana, ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwishoni mwa mwezi Agosti 2021, wakati Gantz alipoyatembelea makao makuu ya Mamlaka ya Palestina katika mji wa Ramallah, Ukingo wa Magharibi, ukiwa mkutano wa kwanza rasmi wa kiwango hicho kwa miaka kadhaa.
dpa, ap, afp, reuters