ADF yafanya mashambulizi mapya Kongo
30 Januari 2023Shambulio la jana ni miongoni mwa mashambulizi yanayofanywa na ADF kila uchao katika eneo hilo la kaskazini mashariki ya Congo.
Mauwaji hayo yalifanywa na ADF katika utawala wa Walese Vunkutu, katika eneo ambako wakaazi walikuwa wameanza kurudi makwao, baada ya kukimbilia maeneo mengine, kutafuta usalama.
Ripoti ya mauwaji ya jana ilithibitishwa na mjumbe wa gavana wa Ituri katika utawala wa Walese Vunkutu Moïse Utsini kwa njia ya simu.
"Eneo letu limepigwa na mushtuko. Kuna watu waliouawa katika vijiji vitatu."
Aliongeza kwamba miongoni mwa vijiji ambavyo vimeshambuliwa ni pamoja Ofayi, Manyala na Bandindese.
Soma zaidi:Mlipuko wa bomu wajeruhi watu 17 nchini Kongo
Alisema katika mapambano hayo baadhi ya wapiganaji wa kundi laADF waliuwawa na silaha zao kuchukuliwakatika eneo la Mapipi huko Bandindese.
"Afadhali hapo Bandindese kwani kuna ADF wawili waliouawa na silaha zao mbili kuchukuliwa"
Watetezi wa haki za binadamu walaani mashambulizi
Mratibu wa shirika la kutetea haki za binadamu CRDH kitengo chake cha Irumu Christophe Munyanderu,ameiambia Dw kwamba kunataarifa kwa kundi hilo la wapiganaji kujenga kambi katika eneo la Magharibi.
Alisema mashirika yote ya kutetea haki za binadamu katika eneo hilo yamesikitishwa na kulaani kuuwawa kwa watu kadhaahuku miili yao haijulikani ilipo.
"ADF,wamejenga kambi zao eneo la magharibi, na huko ndiko wanakotikea kwenda kuwauwa watu katika eneo la mashariki ya Irumu." Alisema Munyanderu.
Soma zaidi:Uganda yapuuza ripoti ya UN kuhusu operesheni yake Kongo
Katika kile alichokisema kuzuia mauaji zaidi katika siku za usoni ameyatolea mwito majeshi ya muungano yaani UPDF na FARDC, kuanzisha operesheni katika eneo la magharibi, ilikubomoa kambi muhimu za ADF huko.
M23 nao waendeleza mashambulizi
Wakati magaidi ADF kutoka Uganda wanaendelea kuwauwa watu katika wilaya za Beni, Irumu na Mambasa, nao waasi wa M23 wanaendelea na mapigano katika wilaya ya Masisi.
Milio ya risasi imekuwa ikisikika katika kijiji cha Kyahemba, kilomita sita mashariki ya Kitchanga, ambako M23 wanayo nia ya kukata barabara inayotoka Mweso kwenda Nyanzale na malengo yao nikukiteka kijiji cha Mweso.
Soma zaidi:M23 wazidi kuteka maeneo mashariki ya Kongo
Hali hiyo ya mapigano, imewapelekea baadhi ya wakaazi wa Mweso kukihama kijiji chao, na kukimbilia katika wilaya jirani ya Walikale, katika kijiji cha Pinga, zadokeza duru toka huko.
Nazo duru karibu najeshi la Kongo zadokeza, kwamba jeshi la FARDC linafanya juu chini, ilikukiteka upya kijiji cha Kitchanga, kilichoanguka mikononi mwa M23 wiki iliyopita.
Wakati hali tete ya kiusalama ikishuhudiwa katika maeneo kadhaa nchini Kongo,Juhudi za kusaka amani zinazofanywa na jumuia za kimataifa na kikanda bado hazijaleta matokeo chanya.