AfD yachomoza uchaguzi wa jimbo la Saxony
1 Septemba 2014Chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU kiliibuka mshindi katika uchaguzi huo, lakini sasa kinahitaji mshirika mpya wa kuunda naye serikali baada ya chama cha Kiliberali FDP kushindwa tena kupeleka wawakilishi katika bunge la jimbo hilo.
Matokeo ya awali ya uchaguzi yanaonyesha kuwa chama cha Kansela Merkel cha CDU kilipata asilimia 39.4 ikiwa ni karibu asilimia moja chini ya matokeo yake ya mwaka 2009, na mabaya zaidi tangu Ujerumani mbili zilipoungana tena mwaka 1990.
Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke, kilimaliza kwa mbali katika nafasi ya pili kikiwa na asilimia 18.9, ambayo pia ni pungufu kidogo ya matokeo yake ya miaka mitano iliyopita.
Pigo jingine kwa FDP
Lakini muhimu zaidi katika uchaguzi huo, ni ukweli kwamba chama cha Kiliberali FDP ambacho kilikuwa mshirika mdogo katika serikali ya muungano ya waziri mkuu Stanislaw Tillich wa CDU kwenye jimbo hilo, kilishindwa kuvuka kihunzi cha asilimia 5 ya kura inayohitajika kupeleka wawakilishi bungeni.
Hili ndiyo pigo la hivi karibuni kwa chama hicho, ambacho pia kilishindwa kupeleka wawakilishi katika bunge la shirikisho Bundestag, katika uchaguzi mkuu uliyofanyika Septemba mwaka jana.
Matokeo mabaya ya chama FDP yanamaanisha kuwa waziri mkuu Tillich anatafuta mshirika mpya wa kuunda naye serikali kwa sababu licha ya ukweli kwamba chama chake cha CDU kimepata matokeo mazuri, lakini hayakipi wingi wa kutosha kuweza kuongoza chenyewe.
AfD yajifaragua
Muhimu pia katika uchaguzi huu ni ukweli kwamba chama kinachoupinga Umoja wa Ulaya cha AfD kilifanikiwa kuvuka kihunzi cha asilimia 5 kwa kupata asilimia 9.7, hii ikimaanisha kuwa kimeshinda viti vyake vya kwanza kabisaa katika uchaguzi wa majimbo nchini Ujerumani.
"Ni matokea mazuri kabisaa, na tumeridhika nayo kwa sababu yemeonyesha kuwa chama cha AfD sasa kimeingia rasmi katika mfumo wa vyama vya siasa vya Ujerumani, na kwamba tumepata imani kubwa ya wapiga kura wa Saxony," alisema Profesa Bernd Lucke, mwanzilishi wa AfD, ambaye huko nyuma alikuwa mwanachama wa CDU.
Chama cha Kisoshalisti SPD ambacho ni mshirika wa Kansela Angela Merkel katika serikali ya kuu ya muungano ya Ujerumani kilipata asilimia 12.4 hii ikiwa asilimia 2 zaidi ya kilivyopata mwaka 2009. Chama cha Kijani nacho kitakuwa na wawakilishi katika bunge hilo jipya la jimbo la Saxony, baada ya kupata asilimia 5.7 wakati chama cha mrengo mkali wa kulia cha NPD kilishindwa kuingia bungeni baada ya kuambulia asilimia 4.9 ya kura.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpa,rtre,DW
Mhariri: Saum Yusuf