1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa chama cha upinzani nchini Ethiopia auawa

10 Aprili 2024

Afisa mmoja wa chama cha upinzani cha Oromo Liberation Front (OLF) nchini Ethiopia Bate Urgessa, amepatikana akiwa ameuawa kwa kupigwa risasi, saa chache baada ya kukamatwa na vikosi vya serikali.

https://p.dw.com/p/4edbJ
Oromo Liberation Front (OLF)
Nembo ya chama cha upinzani cha Oromo Liberation Front (OLF)Picha: Seyoum Getu/DW

Mwezi uliopita, Urgessa mwenye umri wa miaka 41, aliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kuwekwa kizuizini pamoja na mwandishi habari wa Ufaransa Antoine Galindo.

Msemaji wa Olf Lemi Gemechu ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Bate alikamatwa tena na vikosi vya serikali katika hoteli moja mjini Meki iliyoko umbali wa kilomita 150 Kusini mwa Addis Ababa.

Gemechu amesema familia ya Bate imethibitisha kwamba mwili wake ulipatikana leo kando ya barabara moja ya eneo la Melissa viungani mwa mji wa Meki na kuongeza kuwa alikuwa amepigwa risasi.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Ethiopia lilizihimiza serikali zote za mikoa na kitaifa kufanya uchunguzi wa haraka na kina kuhusu mauaji hayo.