Africa mwaka 2021: Mapitio katika picha
Kuanzia ushindi wa muziki wa rumba wa nchini Congo hadi mapinduzi yaliyotikisa bara zima, tunarudi nyuma kuangazia mapito ya kisiasa, tamaduni na hata jamii barani Afrika kwa mwaka 2021.
Tanzania yabadili msimamo kuhusu corona
Mapema baada tu ya kuibuka kwa janga la COVID-19, rais wa Tanzania wa wakati huo John Magufuli alitangaza nchi yake "iko salama" huku akimshukuru Mungu kwa kuwaepusha na janga hilo. Lakini alipofariki mwezi Machi, mrithi wake, Samia Suluhu Hassan alibadili sera hii. Alianzisha kikosi kazi cha COVID, akazindua mpango wa chanjo na yeye mwenyewe akchapisha picha akipata chanjo.
Historia yaandikwa WTO
Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria alipigiwa kura kuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara Duniani WTO mwezi Machi na kuwa mwanamke na Mwafrika wa kwanza kuliongoza shirika hilo. Okonjo-Iweala ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha, alikuwa mwenyekiti wa zamani wa bodi ya GAVI, muungano wa chanjo na aliwahi kuwa waziri wa fedha wa Nigeria mara mbili.
Mapinduzi ya Chad
Idriss Deby wa Chad anayepiga kura alikuwa tu amechaguliwa kuwa rais kwa muhula wa sita lakini alipigwa risasi na kuuawa mwezi Aprili wakati wa mapigano na waasi. Utawala wake uligubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, ufisadi na upendeleo. Baada ya kifo chake majenerali wa jeshi walimweka mwanawe Mahamat kama kiongozi wa mpito katika kile ambacho wengi wamekiita "mapinduzi ya kifalme.
Mapinduzi, mapinduzi na mapinduzi zaidi
Mamady Doumbouya (anayepunga mkono) wa Guinea ni mmoja tu wa viongozi wa kijeshi waliochukua madaraka kwa nguvu mwaka 2021. Mapema mwaka huu jeshi la Mali lilifanya mapinduzi ya pili katika kipindi cha miezi tisa. Nchini Sudan wanajeshi waliwaondoa viongozi wa kiraia katika makubaliano ya kugawana madaraka na kutangaza hali ya hatari mwezi Oktoba na kusababisha maandamano makubwa.
Wakimbizwa na volkano ya ghafla
Mlima Nyiragongo nchini Kongo ulipolipuka mwezi wa Mei, maelfu ya watu waliokuwa wakiishi chini ya mlima huo wa volcano walilazimika kukimbia ghafla. Zaidi ya nyumba 3,000 zilichomwa na kusalia majivu. Ofisi ya iliyoendesha mfumo wa kutoa tahadhari mapema ilisema serikali imeshindwa kutoa ufadhili wa kutosha kwa ajili ya kuufuatilia mlima huo.
Operesheni ya pamoja, Msumbiji
Mwezi Septemba rais wa Rwanda Paul Kagame (katikati kushoto) alitembelea wanajeshi wa Rwanda waliojiunga na mapambano dhidi ya makundi ya Kiislam katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi (katikati kulia) alipongeza "mshikamano" wa majeshi ya Rwanda. Wanajeshi kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pia wanashiriki katika operesheni hiyo ya pamoja.
Vita vyaendelea kuwatesa raia wa jimbo la Tigray
Nchini Ethiopia, matumaini ya kufikia mwafaka wa kusitisha mapigano yanafifia kabla ya mwisho wa mwaka huu kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na wapiganaji wa Tigray. Vita vya raia vilivyoanza Novemba 2020 vimesababisha maelfu ya watu kuuawa, zaidi ya watu milioni 2 kulazimika kuyahama makazi yao na kuona visa vingi vya mateso kwa raia, kama unavyomuona msichana huyu wa miaka 17.
Afrika Kusini ilitengwa
Afrika Kusini imetengwa na sehemu nyingi za dunia baada ya wanasayansi nchini humo kurekodi kisa cha kwanza cha aina mpya ya kirusi cha corona aina ya omicron mwishoni mwa mwezi Novemba. Zaidi ya mataifa kumi na mbili yalisitisha safari za ndege kutoka Afrika Kusini. Ingawa mataifa mengine, kama Uingereza yameondoa marufuku yao kwa wasafiri wa Afrika Kusini, lakini mataifa mengine bado yameizuia.
Jamii ilishangilia kurejeshwa kwa urithi wa kiafrika ulioibwa
2021 kulishuhudiwa mabadiliko baada ya mataifa kama Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji na Uholanzi kurejesha urithi wa kitamaduni wa Kiafrika. Mataifa hayo ndio yaliyoanza kurejesha kazi za sanaa zilizoibwa katika enzi ya ukoloni na mengine yameahidi kufanya hivyo. Kiti cha enzi cha Mfalme Ghezo wa Dahomey hatimaye kilirejeshwa Benin kutoka Paris na kupokelewa kwa heshima kubwa ya kijeshi.
Ufaransa ilipojiondoa, Mali ikashika usukani
Ufaransa imekabidhi kambi yake ya Timbuktu kaskazini mwa Mali kwa wanajeshi wa Mali baada ya miaka tisa ya kupambana na waasi wa Kiislamu. Ufaransa imesema itawaondoa zaidi ya wanajeshi wake 2,000 kutoka Sahel mwaka 2022. Katika mahojiano na DW, waziri wa mambo ya nje wa Mali alisema anataka mazungumzo ya wazi na yenye kujenga na Ufaransa lakini Mali inahitaji kuwa na vifaa ili kushika usukani.
Mwaka wa mafanikio kwenye fasihi
Ulikuwa mwaka mzuri kwa waandishi wa Kiafrika. Tsitsi Dangarembga wa Zimbabwe (pichani) alitunukiwa Tuzo ya mwaka ya Amani ya Biashara ya Vitabu ya Ujerumani, Mohamed Mbougar Sarr wa Senegal alichukua Prix Goncourt ya Ufaransa na wa Afrika Kusini Damon Galgut alishinda Tuzo ya Booker ya ubunifu. Juu ya yote mwandishi Mtanzania Abdulrazak Gurnah alishinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka wa 2021.
Muziki nao ulikuwemo!
Rumba ya Afrika inapendwa katika bara zima. Lakini kwa Wakongo, nchini Kongo na Jamhuri ya Kongo, rumba ni zaidi ya muziki - huashiria sherehe na maombolezo. Na UNESCO sasa imeuongeza muziki wa rumba wa Congo kwenye orodha yake ya urithi miaka mitano baada ya kifo cha mwanamuziki nguli wa Rumba Papa Wemba (pichani hapa 2006). Hatua hiyo iliibua furaha katika nchi zote mbili.