1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika imejipangaje kukabiliana na Monsanto na Bayer?

20 Septemba 2016

Baada ya kampuni ya Ujerumani Bayer kuinunua kampuni ya Monsanto ya Marekani, Bayer italidhibiti soko la mbegu na dawa za kunyunyizia mimea. Mashirika ya misaada yana hofu juu ya hali ya soko la kilimo.

https://p.dw.com/p/1K5HJ
Bild-Kombo Bayer Monsanto

Mkurugenzi wa Kituo cha Uhai Anuwai nchini Afrika ya Kusini, ACB, Mariam Mayet, anasema si habari nzuri kwa Afrika kwamba kampuni za Monsanto na Bayer zimeungana, maana hii inamaanisha kuwa sasa lile shinikizo la kutumia kemikali kwenye kilimo barani Afrika litaongezeka. "Nafikiri tutaziona serikali za Afrika zikisukumwa kwenye shinikizo la kutumia kemikali na mbegu zilizobadilishwa asili yake na hasa katika mazao ya mahindi, maharage ya soya na pamba."

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambako kilimo cha kutumia mbegu zilizobadilishwa asili yake kinaruhusiwa, na mtaalamu huyo anasema tayari kampuni ya Monsanto inalidhibiti soko la mbegu za mahindi nchini mwake na katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.

Kampuni zenye kulitawala soko

Kwa mujibu wa Mariam Mayet kampuni hizo mbili zitakuwa shirika mojawapo kubwa litakalodhibiti takribani asilimia 30 ya soko la mbegu na karibu robo ya soko la kemikali za kunyunyizia mimea duniani. Nchi nyingi za Afrika zinategemea mbegu na dawa za kunyunyizia katika harakati za kupambana na njaa. Hata hivyo, mashirika ya misaada yanahofia kwamba nchi masikini hazitakuwa na uwezo wa kujihami dhidi ya makampuni makubwa ya kilimo, na kununuliwa huko kwa kampuni ya Monsanto na kampuni ya Bayer ya Ujerumani ni hatua inayomaanisha hatari kubwa kwa wakulima barani Afrika.

Juu ya hatari hizo, huyu hapa Katibu Mkuu wa shirika la misaada la Care International, Wolfgang Jamann. "Tunafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hatua ya kuungana makampuni ya Bayer na Monsanto, hatua kama hii maana yake ni kushindikana kupatikana suluhisho katika maswala ya kilimo. Asilimia 60 ya soko la mbegu linadhibitiwa na makampuni makubwa 6 ya kilimo duniani, wakulima wadogo wadogo wanahitaji masuluhisho tafauti ambayo hayawezi kutimizwa na makampuni ya Bayer na Monsanto." Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba masuluhisho ya kampuni hizo kubwa yanawahusu hasa wakulima wa Marekani na wa barani Ulaya.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi wa Kituo cha Uhai Anuwai nchini Afrika ya Kusini, Mariam Mayet, ametahadharisha juu ya uwezekano wa kupanda kwa bei za mbegu kutokana na ushindani mdogo kwenye soko. Katika nchi nyingi za Afrika, sehemu kubwa ya kilimo inaendeshwa na wakulima wadogo wadogo ambao wanapata kiasi kidogo cha fedha kutokana na mazao yao. Bei ya juu ya mbegu itawafanya wakulima washindwe kuendelea na shughuli za kilimo.

Shamba la mahindi yaliyooteshwa na mbegu za Monsanto
Shamba la mahindi yaliyooteshwa na mbegu za MonsantoPicha: picture alliance/dpa/Fotografia/R. Pera

Kwa kila hali, wachambuzi wa masuala ya usalama wa chakula wanaona kuwa kampuni ya Bayer imejiingiza kwenye matatizo kutokana na kuinunua kampuni ya Monsanto, kwani kampuni hiyo ya Marekani ina sifa mbaya duniani kote. Ushahidi ni kampuni hiyo ilipowauzia wakulima wa Burkina Faso mbegu za pamba zilizobadilishwa asili yake, lakini ikafahamika baadaye kuwa mbegu hizo hazikuwa na ubora uliotakikana.

Mwandishi: Antonio Cascais
Tafsiri: Zainab Aziz
Mhariri: Mohammed Khelef