1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni ashika kani

19 Februari 2016

Magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii yameandika juu ya uchaguzi wa Uganda na juu ya biashara haramu ya mbao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

https://p.dw.com/p/1HylF
Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: picture alliance/Kyodo

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine"linasema baada ya kuwamo madarakani kwa muda wa miaka 30 Rais Yoweri Museveni wa Uganda bado anang'ang'ania madaraka. Gazeti la "Süddeutsche" linatupasha habari juu ya wahalifu wanaoimaliza misitu katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" Ujerumani wiki hii litahadharisha tena juu ya hatari ya kutokea njaa katika nchi kadhaa za Afrika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Gazeti hilo linasema watu zaidi ya Milioni 45 karibuni tu watategemea misaada ya chakula kutoka nje.

Uchaguzi mkuu umefanyika nchini Uganda ambapo wagombea wakuu walikuwa Rais Yoweri Museveni, Dr. Kizze Besyige na Amama Mbabazi. Katika makala yake juu ya uchaguzi huo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema licha ya kuwamo madarakani kwa miaka 30 Museveni bado amenata kwenye kiti.Hataki kubanduka.

Gazeti hilo linaeleza kwamba katika kipindi cha miaka 30 madarakani Museveni amejenga mfumo wa madaraka unaohakikisha kwamba anadhibiti kila takriban nyanja zote za jamii . Museveni anadhibiti pia bajeti za majimbo.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" linaarifu kwamba alipoenda kuhutubia kwenye mkutano wa kampeni yake ya uchaguzi, katika mji wa Kawempe, kaskazini ya mji mkuu wa Uganda, Kampala, Museveni aliwalaumu wapiga kura kwa kusababisha sehemu yao iwe nyuma katika maendeleo.

Gazeti hilo limemnukulu Museveni akisema kwamba watu hao walimchagua mgombea wa chama cha upinzani katika uchaguzi uliopita na ndiyo sababu vitega uchumi havikupelekwa katika jimbo lao.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema njia nyingine inayotumiwa na Museveni ili kujihakikishia madaraka ni kudhibiti vyombo vya habari. Vituo vya radio kadhaa vilifungwa katika wiki zilizopita baada ya kutangaza mahojiano na wagombea wa upinzani.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linazungumzia juu ya mwito uliotolewa na aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kwenye mkutano wa masuala ya usalama uliofanyika hivi karibuni katika mji wa Munic- kusini mwa Ujerumani. Katika mwito huo Kofi Annan amezitaka nchi tajiri zifanye juhudi zaidi ili kuwasaidia vijana wa Afrika.

Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan
Aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi AnnanPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Annan amekaririwa akitahadharisha kwamba karibuni tu, vijana wa Afrika zaidi Milioni 11 , kila mwaka watasongamana katika kutafuta nafasi za ajira. Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema, migogoro mingi iliyoko barani Afrika, inaonyesha nini kinaweza kutokea ikiwa vijana hao watazubaa zubaa bila ya ajira.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limemnukulu Katibu Mkuu huyo wa zamani akieleza kuwa, ukosefu wa ajira unaweza kuwa rutuba ya kustawisha itikadi kali za makundi ya kigaidi kama ya Al-Shabaab na Boko Haram.

Gazeti la Süddeutsche" wiki hii linazumgumzia juu ya biashara haramu ya kukata miti katika misitu ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo. Gazeti hilo linasema ripoti inabainisha kwamba mbao zinazosafirishwa na wahalifu zinaingia katika masoko ya Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Umoja wa Ulaya umeshindwa kuzuia biashara hiyo haramu licha wa kuwapo sheria . Gazeti la "Süddeutsche" linaarifu kwamba sheria ya kuzuia biashara haramu ya mbao ilipitishwa na Umoja wa Ulaya, mnamo mwaka wa 2010 na ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka wa 2013.

Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti iliyokaririwa na gazeti hilo, sheria hiyo haifanyi kazi kwa sababu hakuna motisha miongoni mwa wahusika na wala hakuna habari juu yake. Kwa mujibu wa gazeti la "Süddeutsche "ukataji miti unachangia hadi asilimia 5 katika kuongezeka kiwango cha joto duniani.

Gazeti hilo pia limefahamisha kwamba wahalifu wanachuma kati ya dola Bilioni 30 hadi 100 kwa kufanya biashara haramu ya mbao. Gazeti la "Süddeutsche" pia limefahamisha kwamba, takwimu ambazo bado hazijatolewa hadharani zinaonyesha kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshasafirisha mbao kwenda Umoja wa Ulaya zenye thamani ya dola Milioni 64 kuanzia mwaka 2013.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Gakuba Daniel