Zuma atangaza sera mpya kuukabili mgogoro wa uchumi
29 Februari 2016Gazeti la "Süddeutsche" linasema Rais Yoweri Musevi amepata muhula mwingine wa miaka mitano baada ya kuwamo katika madaraka kuwa muda wa miaka 30 nchini Uganda.
Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Museveni alitangazwa mshindi na tume ya uchaguzi, huku yakiwepo madai ya wizi wa kura. "Süddeutsche limemnukulu Museveni akiwashukuru watu waliompa tena imani yao kwa mara nyingine.
Gazeti hilo limewanukulu wajumbe wa Umoja wa Afrika waliosimamia uchaguzi wakisema kwa ujumla uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.Hata hivyo wajumbe hao walilalamika kwamba katika vituo kadhaa vya kupigia kura vifaa vilicheleweshwa.
Wajumbe hao wamekaririwa na gazeti la "Süddeutsche" wakisema karatasi za kupigia kura pia hazikupelekwa kwa wakati uliopangwa. Gazeti hilo pia linatilia maanani kuwa baada ya Museveni kutangazwa mshindi shangwe hazikujitokeza sana..Badala yake askari waliokuwa wameshamiri kwa silaha walijaa barabarani.
Zuma apania kuzuia kuporomoka kwa sarafu ya Rand
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ametingwa na mgogoro mkubwa wa kiasi kwamba sasa kilichobakia kwake kufanya ni kujitetea. Zuma amesema jambo la kipaumbele kwake sasa ni kuzuia kuendelea kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Rand
Gazeti "Süddeutsche" linasema Afrika Kusini imo hatarini kukumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Dalili zinaonyesha huenda uchumi wa nchi hiyo ukashuka.
Hata hivyo gazeti hilo limemnukulu Rais Zuma akiazimia kuchukua hatua ili kuiimarisha sarafu ya Rand na kurejesha imani, kwenye masoko ya fedha kwamba Afrika Kusini inao uwezo wa kulipa mikopo.
Gazeti la "Süddeutsche" linakumbusha kwamba ni hivi karibuni tu ambapo Rais Zuma aliwataka wananchi wake waache kutia chumvi wanapozungumzia matatizo ya nchi yao. Lakini sasa ,gazeti hilo linasema matatizo ya Afrika Kusini yamefikia kiwango cha kumnyima raha Rais Zuma.Sasa hawezi tena kutabasamu na kufanya mizaha anapojibu maswali juu ya hali ya nchi yake.
Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba mahitaji ya malighafi yamepungua duniani. Linaeleza kwamba China, ambayo ni mnunuzi mkuu wa malighafi imepunguza manunuzi. Gazeti hilo pia limeeleza kuwa kwa muda mrefu Afrika kusini imekumbwa na ukame.Kutokana na sababu hizo mbili uchumi wa Afrika Kusini umo katika hatari ya kuingia katika mdororo.
Mgogoro wa wakimbizi unaendelea kuwa changamoto kwa nchi za Ulaya
Hizo ni habari zilizoandikwa wiki hii na gazeti la "Der Tagesspiegel" Gazeti hilo linaarifu kwamba Uhispania inaamini kuwa imepata njia ya ufanisi katika kupunguza wakimbizi wanaotokea nchi za Afrika magharibi.
Gazeti hilo limeeleza kuwa Uhispania itazishauri nchi nyingine za Umoja wa Ulaya nazo ziitumie njia hiyo. Gazeti la "Der Tagesspiegel" linafahamisha kuwa mkakati huo wa Uhispania ni wa mambo matatu.
Kwanza kuzuia njia zinazotumiwa na wakimbizi ili kufika Ulaya. Pili kuwafukuza haraka wahamiaji na wakimbizi wanaoingia kinyume cha sheria na tatu kupeleka misaada ya maendeleo kwa nchi ambako wakimbizi wanatokea - Afrika magharibi.
Waziri Mkuu wa Uhispania Mario Rajoy amenukuliwa na gazeti la "Der Tagesspiegel" akiwaambia viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya kwamba nchi yake imefanikiwa katika kuushughulikia mgogoro wa wakimbizi.
Gazeti hilo limeripoti kwamba idara ya Umoja wa Ulaya ya ulinzi wa mipaka, Frontex imeipongeza Uhispania kwa kufunga njia ya Afrika magharibi inayotumiwa na wakimbizi.
.
Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen:
Mhariri:Josephat Charo