Afrika katika magazeti ya Ujerumani
9 Aprili 2021Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika mengi kuhusu bara la Afrika ikiwemo hatua ya jeshi la Msumbiji ya kuudhibiti mji wa Palma uliokuwa ukishikiliwa na waasi. Pia yameangazia mwenendo wa janga la corona nchini ya Afrika ya Kusini na mapokeo ya chanjo dhidi ya virusi hivyo.
die Tageszeitung
Gazeti la die Tageszeitung ambalo limeandika kuwa jeshi la Msumbiji lilifanikiwa kuudhibiti mji wa Palma kutoka kwa waasi wenye itikadi kali. Mji huo umeharibiwa vibaya, wakaazi wengi wamelazimika kuukimbia huku maelfu wakibaki bila huduma muhimu.
Gazeti hilo limeandika, zaidi ya watu 110,000 ambao kwa mujibu wa umoja wa mataifa walikuwa wakiishi Palma hapo awali hawajulikani walipo. Kwa mujibu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya kiutu za Umoja wa mataifa OCHA, hadi Aprili mosi mwaka huu, watu 9,158 kutoka Palma waliandikishwa na mashirika ya misaada ya dharura katika maeneo jirani wengi wao wakiwa wamedhoofu sana. Wengi wa waliopoteza makazi yao bado wanahofu wakikumbuka waliyoyaona.
Ofisi hiyo ya uratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja wa mataifa inasema zipo taarifa kuwa maelfu ya watu bado wamejificha vichakani karibu na Palma wakiwa hawana maji wala chakula. Serikali ya Msumbiji hata hivyo inasema baada ya wanajeshi kuudhibiti mji wa Palma wakimbizi wanaweza kurudi kwenye kwenye mji huo.
Neue Zürcher
Tukisalia nchini Msumbiji, gazeti la Neue Zürcher limeandika kuhusu hatua ya kampuni ya mafuta ya Total ya kusimamisha shughuli zake nchini humo kutokana na mashambulizi ya waasi. Kampuni hiyo ya mafuta ya Ufaransa iliwaondoa wafanyakazi wake wote kutoka katika ofisi zake huko kaskazini mashariki mwa Msumbiji Ijumaa iliyopita na ilisimamisha mradi wa mabilioni ya dola. Total iliamua kufunga shughuli zake baada ya camera za ulinzi kuonesha wafuasi wa kundi la waasi wenye itikadi kali la Ahlu Sunna wal Jamaa wakiwa karibu na moja ya mitambo yao huko Afungi.
Makundi ya waasi wenye itikadi kali yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika vijiji na miji kaskazini Mashariki mwa Msumbiji kwa zaidi ya maka mitatu lakini kamwe mashambulizi hayo hayakuwahi kufika karibu na maeneo ya uchimbaji mafuta kama hivi sasa.
Neues Deuchland
Neues Deuchland liliangazia Zambia na jinsi madeni yake makubwa yanavyozipa nafasi taasisi za fedha nafasi za kucheza nayo namna zinavyotaka. Taasisi hizo ni pamoja na Shirika la fedha la kimataifa IMF, watoa mikopo binafsi na China.
Zambia ilitangaza kuwa iimeshindwa kulipa madeni ikiwa athari za uchumi wake zilizotokana na janga la corna. Gazeti la Neues Deutschland linaenda mbele zaidi na kusema kuwa kwa sasa, mambo hayasongi mbele Zambia. Ujenzi wa uwanja wa ndege karibu na Ndola unasuasua na hivi karibuni, Jumapili ya Pasaka, katika hali ya kushangaza kwa wafanyakazi wa ujenzi katika eneo hilo, walishuhudia ndege ya mizigo ikitua kwenye uwanja huo wa ndege ambao haujakamilika.
Gazeti hili linaandika kuwa uchumi wa Zambia unakabiliwa changamoto na kushuka kwa bei za malighafi kunakoiweka nchi hiyo katika shinikizo kubwa. Ili kuziba mianya kwenye bajeti, Zambia ililazimika kuchukua mikopo mipya. Uhusiano kati ya janga la corona, bei za malighafi na kutumbukia kwenye deni kubwa kumesababisha Zambia kushindwa kulipa madeni na wadai binafsi kamwe hawatoshiriki kutoa msamaha wa madeni.
Frankfuter Allgemeine
Gazeti la Frankfuter Allgemeine linaimulika hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Afrika ya kusini pamoja na utayari wa watu kupokea chanjo dhidi ya virusi hivyo. Gazeti hilo limeandika kuwa waganga wa jadi nchini humo wanataka kupata chanjo lakini bado wapo wengi ambao hawazitaki.
Zaidi Frankfuter Allgemeine linaandika kuwa waganga wa jadi ni watu muhimu wenye jukumu kubwa katika sekta ya afya nchini humo na linamtolea mfano Yanga Nduku ambaye ni Sangoma, anategemea nguvu za shanga kutibu watu na tiba asili za kiafrika pamoja na ushauri wa mababu zake lakini hivi karibuni alipokea chanjo dhidi ya virusi vya corona kutoka Marekan. Anasema zaidi ya nusu ya watu nchini humo, huanza kuomba ushauri kwa waganga wa jadi juu ya afya zao hivyo baadhi ya Waganga wa jadi wanataka kuonesha mfano mzuri kwa kupata chanjo dhidi ya COVID 19. Hata hivyo wanakabiliwa na changamoto kwani wapo watu wanaofikiri chanjo hizo ni kwa ajili ya kuwaua.