Afrika Kusini yazuia watoto 400 wa Zimbabwe kusafirishwa
4 Desemba 2023Mabasi hayo yamekamatwa wakati wa operesheni maalumu ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu. Kamishna wa shirika la usimamizi wa mipaka la Afrika ya Kusini Mike Masiapato, amethibitisha kuwa Jumamosi usiku waliwapata watoto 443 wenye chini ya umri wa miaka 8 wakisafiri peke yao katika mabasi yaliyokuwa yakitokea Zimbabwe.
Amesema maafisa wa polisi waliyasimamisha na kuyapekua mabasi 42 na kuwakuta watoto hao waliokuwa wakisafirishwa kinyume cha sheria kuingia nchini humo. Mabasi hayo yaliyokamatwa hata hivyo yaliamriwa kurejea Zimbabwe.
Kutokana na tukio hilo, mashirika yanayowawakilisha raia wa kigeni waishio Afrika ya Kusini yamesema kuna uwezekano kuwa watoto waliokuwa kwenye mabasi hayo yaliyokamatwa walikuwa wakipelekwa kuwatembelea wazazi wao wanaoishi nchini humo wakati huu wa msimu wa kuelekea mwisho wa mwaka, suala ambalo mwenyekiti wa jukwaa , la Africa Diaspora Ngqabutho Mabhena, linalowakilisha raia wa kigeni wanaoishi Afrika Kusini, amesema kuwa shirika lake linaamini ni la kawaida wakati wa majira ya mwisho wa mwaka.
Soma hapa: Tanzania lawamani kwa kutozuia utumikishwaji wa watoto
Hata hivyo Mabhena amesema wamekuwa wakiwaasa wazazi hao raia wa Zimbabwe kuhakikisha wanapopanga safari za kuwaalika watoto wao Afrika ya Kusini wanakuwa na vibali vyote vinavyohitajika. Ameongeza kuwa ni uzembe kuwaacha watoto wasafiri na watu wasio wajua na bila ya kuwa na pasi za kusafiria.
Baadhi ya Wazimbabwe wanaishi Afrika ya Kusini wengi wao kinyume cha sheria baada ya kuhamia katika taifa hilo jirani ndani ya miaka 15 iliyopita wakikimbia hali ngumu ya uchumi ya Zimbabwe.
Soma zaidi: Mtu na mkewe raia wa Marekani washtakiwa Uganda
Kulingana na shirika la habari la AP kuna, karibu raia 178,000 wa Zimbabwe wanafanya kazi na kuishi Afrika ya kusini kisheria chini ya kibali maalumu kinacho wapa msamaha. Licha ya hilo, sensa ya Afrika ya Kusini ya mwaka 2022 ilionesha kwamba kuwa zaidi ya Wazimbabwe milioni moja nchini humo. Badhi ya watu wanakadiria kuwa idadi ya raia hao wa Zimbabwe ni watu milioni tatu katika taifa hilo.
Afrika ya Kusini moja ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi katika bara la Afrika iliunda kikosi kipya cha kusimamia mipaka mnamo mwezi Oktoba. Madhumuni ya kuundwa kwa kikosi hicho ni kukabiliana na uhamiaji haramu kutoka Zimbabwe pamoja na mataifa mengine.