1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika na utatuzi wa matatizo ya Nishati ya Umeme.

Scholastica Mazula5 Juni 2008

Kutatua matatizo ya umeme barani Afrika kutahitaji matumizi ya ufanisi mkubwa wa nishati na nchi kutumia vyema rasilimali zinazoweza kutumika upya.

https://p.dw.com/p/EEH4
Mitambo ya kuzalisha Umeme kwa nguvu za Nyuklia nchini China.Picha: AP

Hii ni kwa mujibu wa Kongamano la Kimataifa la kiuchumi linaloendelea mjini Capetown,Afrika Kusini katika kuliendeleza Bara la Afrika.

Bara la Afrika ambalo watu wake kiasi cha milioni mia sita bado wanaendelea kukosa huduma ya Umeme, linapaswa kufikiria njia bora yakuongeza ufanisi katika masuala ya Umeme, na pia kuthibiti watu wanaojaribu kuiba nishati hiyo kutoka kwenye mitambo yake.

Pierre Gadonneix, ni Mkuu wa Kampuni moja ya Umeme nchini Ufaransa, ambayo ni moja yakampuni kubwa za Nishati hiyo barani ulaya amewaambia wajumbe katika Kongamano hilo Mjini Capetown kuwa Bara la Afrika linaufumbuzi wa aina yake wa vyanzo vingi vya nishati vinavyoweza kutumika upya mikononi mwake.

Amesema ni wazi kwamba hakuna rasilimali nyingi zinazoweza kutumika upya barani Afrika wakati ambapo unafikiria juu ya kitu gani kinawezekana kwakutumia upepo ama Jua, kwa sababu kuna nchi nyingi sana ambazo hazina utaratibu wa kutumia rasilimali za zamani zinazoweza kutumika upya.

Nchini Afrika Kusini Shirika la Umeme la Eskom, limeendelea kuwa katika wakati mgumu ikiwa ni matokeo ya miaka na miaka ya kushindwa kuwekeza katika Nishati ya Umeme kitendo kilichosababisha kuwepo hali ya kiza na viwanda vingi kushindwa kujiendesha.

Mkurugenzi wa Eskom Jacob Maroga, ambaye kampuni yake inajaribu kuongeza gharama kwa asilimia hamsini na tatu, amesema kwamba idara ya Nishati ya Umeme ilitakiwa kuwa na viwango vizuri vya umeme kwa kuangalia ushindani na uwekezaji zaidi kutoka kwenye Makampuni ya watu binafsi.

Bwana Maroga, anasema kwamba anadhani tatizo kubwa lililoko Afrika Kusini ni ukosefu wa bidhaa lakini endapo utauliza kuwa ni kitu gani kati ya vitu vyote kinapatikana kwa bei ndogo basi jibu litakuwa ni Umeme.

Anasema katika mazingira ambayo watu wanakuwa na bidhaa fulani ambayo haipatikani kiurahisi lazima itauzwa kwa bei ya juu.

Kwa upande mwingine, Pierre Gadonneix anasema Nishati ya Umeme haikuwa bidhaa kama ilivyo katika maeneo mengine ambako ushindani ulikuwa ukichukua nafasi kama njia nzuri na watu walilazimika kuelewa ukweli kwamba Umeme ulikuwa ni wa gharama.

Amesema Umeme ni wa gharama kwa vyovyote itakavyokuwa utaendelea kuwa ni wagharama na hii ndiyo hali halisi kwa sababu pia mafuta yamepanda bei.

Naye Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka, amesema kuwa njia mbadala ya matumizi ya Nishati ya Umeme ilikuwa ni mafuta na kila mtu alikuwa akitizamia katika hilo.

Aidha amesema pamoja na kwamba dunia inazungumzia kuhusu matumizi ya Rasilimali za zamani zinazoweza kutumika tena jambo ambalo ni sahihi, lakini amewataka wajumbe kufikiria ni wapi watapata rasilimali hizo kwa haraka na kwa bei ya chini.

Ameendelea kusisitiza matumizi ya mafuta ambayo yanagharimu kiasi kidogo na bado ikawa ni njia bora zaidi katika kile ambacho wamekuwa wakikifanya.

Pierre Gadonneix, ameongeza kuwa tatizo kubwa lililokuwepo Afrika ni ukosefu wa Nishati unatokana na ukosefu wa wataalamu, usambazaji au masuala ya ufundi kama vile watu kuiba Umeme katika mitambo ya Nishati hiyo.