1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika ya Kusini yaongeza uzito wa kisiasa kwenye BRICS

13 Aprili 2011

Mkutano wa klabu ya mataifa yanayoinukia kwa kasi kiuchumi, BRICS, umeanza Kusini mwa China huku kwa mara ya kwanza Afrika ya Kusini ikishiriki kama mwanachama kamili kama zilivyo China, Brazil, India na Urusi.

https://p.dw.com/p/10sok
Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma
Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Ingawa kiuchumi haijafikia kiwango cha wanachama wenzake, Afrika ya Kusini ni taifa lenye umuhimu mkubwa kisiasa katika eneo la kusini ya jangwa la Sahara.

Kuingia kwa Afrika ya Kusini kwenye klabu hii kunachukuliwa kama jitihada za wanachama waanzilishi kupata pa kuanzia kwenye eneo hili.

Kama anavyosema mchambuzi wa mambo ya Afrika katika Eurasia Group, Anne Fruhauf, kwa BRICS, hatua hii "ni ya kidiplomasia zaidi kuliko kuwa ya kiuchumi."

Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na mwenzake wa China, Hu Jintao
Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na mwenzake wa China, Hu JintaoPicha: AP

Afrika ya Kusini yenye uchumi wa dola bilioni 285 za Kimarekani na idadi ndogo zaidi ya watu, ambayo ukuwaji wake ni wa asimilia 3 tu, kwa kweli inapwaya kwenye kapu la mataifa manne makubwa yenye masoko yanayoinukia, yaani India, Urusi, China na Brazil.

Uchumi wa Afrika ya Kusini ni chini ya robo ya uchumi wa Urusi, ambayo ndiyo ndogo kabisa katika mataifa haya ya BRICS. Ambapo unaweza kuwa ni uchumi mkubwa kwa Afrika, huu unakaribiana sana na uchumi wa jimbo moja tu la China.

Lakini Afrika ya Kusini ilipigania kuingia kwenye klabu hii; na ili kupata nafasi, iliishawishi China, ambayo ni mshirika wake mkubwa wa kibiashara, ikichukulia kualikwa kwake kwenye BRICS kulikuwa hatua ya kujitenganisha na kundi la mataifa yenye nafasi ya pili kwenye uchumi unaoinukia.

Alipowasili kwenye mkutano hapo jana (13.04.2011), Rais Jacob Zuma alisema kwamba hicho kilikuwa kipindi cha kihistoria kwa taifa lake. Lakini mwenyekiti wa Goldman Sachs Asset Management, Jim O'Neill, ambaye ndiye aliyebuni jina hili la BRICS hapo mwaka 2001, anasema kuwa Afrika ya Kusini haimo kwenye kundi hili, ambapo wengine wamekuwa wakipendekeza kwamba nchi za Indonesia, Korea ya Kusini na Uturuki ndiyo ambayo yangelistahili zaidi, kwa kuwa uchumi wao ni mkubwa.

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, na mwenzake wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma.
Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, na mwenzake wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma.Picha: AP

Hata hivyo, Afrika ya Kusini inasaidia kujenga daraja la kibiashara baina ya nchi za Kusini na inazisambaza nguvu za klabu ya BRICS na kuweka mizania kati yake na Kundi la Mataifa Saba yenye uchumi mkubwa za Amerika ya Kaskazini na Ulaya ya Magharibi, maarufu kama G7.

Martin Davies ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya Afrika na China na pia mkuu wa taasisi ya Frontier Advisory, anasema kuwa "G7 inawakilisha ulimwengu wa zamani, wakati BRICS inawakilisha ulimwengu wa sasa, na kwa hivyo ili kuifanya ionekane na uwakilishi mpana zaidi, ni lazima kuwa na taifa la Kiafrika linalosema kwa niaba ya dunia inayoendelea."

Kitu chengine ambacho Afrika ya Kusini na mataifa mengine ya kusini mwa Afrika yanaipa klabu ya BRICS ni bidhaa za kulisha mashine zao za viwandani. India, China na Brazil zimekuwa zikifanya jitihada kubwa ya kufanya biashara na Afrika.

Rais mstaafu wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, na Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma
Rais mstaafu wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, na Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob ZumaPicha: AP

Kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Brazil iitwayo Vale inapanga kuwekeza kiasi ya dola bilioni 20 ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo barani Afrika, huku kampuni yake nyengine ya mafuta iitwayo Petrobras ikipanga kuwekeza dola bilioni 3 ifikapo mwaka 2013.

China ilishafanya ubia na mataifa kadhaa ya Kiafrika miongo mingi iliyopita katika mapambano yao ya ukombozi dhidi ya ukoloni, na baadaye ikaanza kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa barabara, skuli, umeme na miundombinu mingine inayosaidia nchi kukua, kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine kuingiza zaidi bidhaa kutoka China.

Huku Afrika ikiendelea, ndivyo pia ilivyo biashara baina yake na China, ambapo shirika la habari la China limeripoti kuwa biashara hii imeongezeka kutoka dola bilioni 10 mwaka 2000 hadi dola bilioni 127 mwaka jana.

Kwa hali hii, ni sawa kusema kuwa Afrika ya Kusini kuingia kwenye klabu ya BRICS, kunaipa fursa zaidi klabu hiyo kujenga himaya yake ya kiuchumi barani Afrika, kuliko kinyume chake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Saumu Ramadhani Mwasimba