1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Afrika yahitaji mabilioni ya majiko salama, IEA

14 Mei 2024

Uchafuzi wa mazingira unapoendelea kusababisha maafa, inakadiriwa kuwa Afrika inahitaji mabilioni ya majiko yanayoendana na mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini je, juhudi hizo zimefikia wapi?

https://p.dw.com/p/4fqbq
Upishi unaotoa moshi mwingi huchafua hewa lakini pia husababisha madhara ya afya kwa watumiaji hasa wanawake.
Upishi unaotoa moshi mwingi huchafua hewa lakini pia husababisha madhara ya afya kwa watumiaji hasa wanawake.Picha: DW

Barani Afrika, msukumo kuelekea upishi unaozingatia hali ya hewa umekuwa nyuma ikilinganishwa na kwingineko ulimwenguni.

Jambo ambalo shirika la Kimataifa la Nishati IEA linatarajia kubadilisha Kwenye mkutano wa kilele unaoendelea huko Paris, unaolenga kukusanya dola bilioni 4 kila mwaka kwa miradi ya upishi kutumia nishati salama kote barani humo.

Kulingana na shirika la IEA, uchafuzi wa hewa kutokana na kupika kwa kutumia nishati chafu huchangia vifo vya mapema vya watu milioni 3.7 duniani kote kila mwaka.

Takriban asilimia 80 ya kaya za Kiafrika au tuseme takriban watu bilioni moja barani Afrika bado wanapika kwa kutumia njia zinazotoa moshi, na gesi chafu kama vile kama vile kuni, mafuta ya taa, mkaa na samadi. Hivi vyote vinachangia mabadiliko ya hali ya hewa na kuathiri afya ya wanawake. Hayo ni kulingana na IEA.

Kaya nyingi barani Afrika hukosa kuwa  na majiko ya kisasa kwa sababu bei zao ni ghali kwa wale wenye mapato ya chini.
Kaya nyingi barani Afrika hukosa kuwa na majiko ya kisasa kwa sababu bei zao ni ghali kwa wale wenye mapato ya chini. Picha: Robin Utrecht/picture alliance

Soma pia: Afrika inaweza kudhibiti soko la malighafi za nishati safi?

Kipato kidogo kwa watu kumudu majiko salama

Aanu Ajayi kutoka Nigeria, mwenye umri wa miaka 39, amekuwa akiuza majiko salama mjini Lagos, huku akiangazia baadhi ya changamoto ambazo hukabili Afrika linapokuja suala la kuachana na njia za zamani za kupika na kukumbatia njia rafiki kwa tabia nchi.

Amelielezea shirika la habari la Reuters kwamba watu wana mashaka na njia za kisasa. Mara nyingi alilazimika kuwaonyesha kivitendo nyumbani na migahawani ndipo watu wanunue angalau majiko machache.

Soma pia: Rais Samia azindua mkakati wa nishati safi Tanzania

Amesema wengi husita kuacha majiko ya kizamani na sufuria za mkaa ambazo wamekuwa wakitumia kwa miongo kadhaa, bila kushawishika kuhusu faida zinazoweza kupatikana kiafya endapo wangekumbatia mbinu za kisasa.

Lakini kikwazo kikubwa kwao ni bei ya majiko ya kisasa. Jiko lake la bei nafuu ni dola 29.58 sawa na naira 42,000. Kiwango hicho ni zaidi ya pato la wastani la kila mwezi nchini humo ambalo ni naira 30,000.

Amesema familia nyingi haziwezi kupata kiasi hicho cha pesa, pasi ya kuweka akiba kidogo kidogo kwa muda wa mwaka mmoja.

Mabara mengine kama Asia na Amerika ya Kusini yaliweka hatua maalum za kuhakikisha majiko ya kisasa yanapatikana kwa urahisi.
Mabara mengine kama Asia na Amerika ya Kusini yaliweka hatua maalum za kuhakikisha majiko ya kisasa yanapatikana kwa urahisi.Picha: DW

Ufadhili mdogo wa mbinu za kisasa za upishi Afrika

Upatikanaji wa nyenzo za kisasa za kupika zisizochafua sana hewa uliongezeka katika mabara mengine ikiwemo Asia na Amerika ya Kusini, lakini ukosefu wa fedha na mipango maalum ya serikali umeiacha Afrika nyuma. Hiyo ni kulingana na IEA.

Soma pia: Matumizi ya nishati mbadala yaongezeka duniani

Shirika hilo limesema usambazaji wa majiko salama bila malipo na ruzuku ya serikali ya mitungi ya gesi ambayo ni nishati safi ilikuwa muhimu kwa mafanikio ya India, China na Indonesia katika kupunguza nusu ya idadi ya watu ambao hawakuwa na nyenzo salama za kupika.

Mkuu wa kitengo cha mageuzi endelevu katika shirika la IEA, Daniel Wetzel aliwaambia wajumbe katika mkutano wa Paris kwamba wanachofikiri kuwa muhimu zaidi ni kupata ishara ya wazi kutoka wakuu wa serikali kwamba suala hilo ni kipaumbele na kwamba wataweka rasilimali maalum kuliwezesha.

Mkutano wa Paris Ufaransa, umewaleta wajumbe kutoka mataifa hamsini, kujadiliana kuhusu nishati salama za kupika chakula duniani.

Je vijana wana uelewa tosha na ushiriki kamili kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi?

Chanzo: Reuters