1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aina ya virusi vya corona kwa mifugo vyaua ngamia Kenya

Michael Kwena/DW Marsabit28 Aprili 2020

Idara ya mifugo katika jimbo la Marsabit Kenya, imeitaka serikali kuangazia mripuko wa virusi vya corona kwa mifugo kwa jina Middle East Respiratory Syndrome (MERS-Cov), ambavyo vimesababisha vifo vya mamia ya ngamia.

https://p.dw.com/p/3bVIN
Kenia Dürre in Wajir 
Picha: DW/Shisia Wasilwa

Idara hiyo imeelezea hofu yake kutokana na ugonjwa huo ambao dalili zake zinalingana na ule wa virusi vya COVID-19.

Wakati ulimwengu ukiendelea kutafuta chanjo dhidi ya virusi vya COVID-19 ambavyo vimepelekea vifo vya zaidi ya watu milioni mbili, jimbo la Marsabit limekuwa la kwanza nchini kuripoti mripuko wa virusi vya MERS-Cov ambavyo huwaathiri mifugo.

Kufikia sasa, mamia ya ngamia wamefariki siku chache baada ya mripuko wa virusi hivyo kuripotiwa.

Katika mkutano na wanahabari mjini Marsabit, afisa mkuu wa idara ya mifugo, Dakta Wario Sori, alisema homa hiyo huenda ikasambaa kote nchini iwapo haitadhibitiwa kwa muda muafaka. Idara hiyo bado haijatoa idadi kamili ya mifugo waliofariki kutokana na homa hiyo ambayo imeathiri pakubwa maeneo ya Turbi-Bubisa, Forole na Badha huri:

"Tuna changamoto wakati huu ambapo ugonjwa umezuka kwa mifugo. Tuna COVID 19 nchini na hivyo virusi vinavyoleta huo ugonjwa pia vinaathiri mifugo. Hapa Marsabit, tuna MERS Cov ambayo inaathiri ngamia. Sisemi kuwa ni virusi vinavyoleta Covid-19 lakini ni familia yake." Amesema Dr. Wario Sori.

Idara hiyo ya mifugo imesema kuwa mripuko wa virusi hivyo vya MERS-Cov huenda ukawakosesha usingizi wakaazi wa Marsabit ambao mara kwa mara wao huwa karibu na mifugo yao.

Mamia ya ngamia wamefariki Marsabit Kenya, kwa kile ambacho madaktari wa mifugo wamesema ni kutokana na aina ya virusi vya corona vinavyowaathiri mifugo.
Mamia ya ngamia wamefariki Marsabit Kenya, kwa kile ambacho madaktari wa mifugo wamesema ni kutokana na aina ya virusi vya corona vinavyowaathiri mifugo.Picha: DW/Shisia Wasilwa

Dakta Wario amedokeza kwamba, wizara ya mifugo inastahili kuweka mbinu maalum za kuitenga mifugo wenye dalili za homa hiyo kwa kuiweka katika karantini ili mifugo mingine isiathirike. Aidha, ametaka afya ya mifugo hiyo kuchunguzwa haraka:

"Lazima tuangalie pia afya ya mifugo yetu kwa sababu jamii ya Marsabit inategemea sana mifugo. Ni jukumu letu kuangalia afya ya mifugo yetu inavyostahili. Kwa sasa watu wanaangazia tu afya ya binadamu na wanasahau afya ya mifugo." Amesema Dr. Wario Sori.ameeleza

Kufikia sasa, Chuo Kikuu cha Washington cha Marekani kwa ushirikiano na idara ya mifugo ya Marsabit inaendelea na utafiti kuhusu virusi hivyo. Ripoti zinaeleza kuwa virusi hivyo vinaweza kusambazwa kutoka kwa mifugo hadi kwa binaadamu.

Dalili za MERS-Cov ni pamoja na homa, kikohozi na upungufu wa pumzi, ambazo ni sawa na za ugonjwa wa COVID-19 ambayo huwaathiri binadamu.