1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Aqsa: Waislamu watilia shaka hatua za Israel

Daniel Gakuba
26 Julai 2017

Kufuatia hatua ya Israel kuondoa mitambo ya kugundua silaha kwenye msikiti wa al-Aqsa mjini Jerusalem, viongozi wa Kiislamu wamesema wataendelea kufanya sala zao nje hadi pale kamati ya kiufundi itakapotoa ripoti kamili.

https://p.dw.com/p/2h9P8
Israel verschärfte Sicherheitsvorkehrungen am Tempelberg in Jerusalem
Waislamu wameendelea kufanya sala zao nje ya mskiti wa al-AqsaPicha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Maafisa wa Israel waliondoa  mitambo hiyo ya kugundua silaha na kamera za video aljafir ya Jumanne, kwa matumaini kuwa hatua hiyo ingeleta utulivu baada ya kipindi cha ghasia za umwagaji damu. Israel imesema badala ya vifaa hivyo, itatafuta suluhisho mbadala la kuhakikisha usalama katika maeneo yanayouzunguka msikiti wa al-Aqsa, ambayo kwa wayahudi yanajulikana kama mlima wa hekalu.

Lakini wapalestina wamesema bado hawakubaliani na mikakati mipya ya usalama. Waziri Mkuu wa Palestina na maimam wa Kiislamu wenye dhamana ya kuulinda msikiti wa al-Aqsa, wamesema wanapinga vikwazo vyote kwa uhuru wa kuabudu, na kutaka hali irejeshwe kikamilifu kama ilivyokuwa kabla ya tarehe 14 Julai ziliporipuka ghasia hizi mpya.

''Tutaendelea kufanya sala zetu nje ya lango la al-Aqsa, na katika mitaa ya Jerusalem, hadi pale uamuzi wa kurudi katika msikiti huo utakapochukuliwa. Tutasubiri kupata ripoti kamili kabla ya kurudi ndani ya msikiti wa al-Aqsa'', Amesema Mohammed Hussein, mmoja wa maimam.

Erdogan aingilia kati

Huku hayo yakiarifiwa, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameingilia kati, na kuionya Israel kuwa ndio itakayoumia zaidi ikiwa itaendeleza mzozo kwenye msikiti wa al-Aqsa. Akizungumza mjini Ankara, Erdogan amesema na hapa namnukuu, ''wanataka kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi, kuutwaa msikiti wa al-Aqsa kutoka mikononi mwa Waislamu, hakuna maelezo mengine''. Mwisho wa kunukuu.

Israel - Palästina - Konflikt - Unruhen
Tangu tarehe 14 Julai, 2017, eneo la mskiti wa al-Aqsa limeshuhudia ghasia za umwagaji damuPicha: Getty Images/AFP/A. Momani

Uamuzi wa Israel kuondoa mitambo ya kugundua silaha na kamera za video ulifikiwa baada ya kikao cha baraza la usalama la Israel ambacho kilidumu kwa saa kadhaa.

Mchango wa Marekani katika kutafuta suluhisho

Balozi wa Marekani nchini Israel David Friedman ambaye ametembelea bunge la Israel, amesema zimefanyika juhudi kubwa za nyuma ya pazia, baina ya Marekani, Israel na Jordan ambayo ndiyo yenye dhamana ya usalama wa maeneo matakatifu ya waislamu mjini Jerusalem.

''Tumeweza kusuluhisha haraka mzozo huu, ambao vinginevyo usingemalizika salama'', amesema balozi huyo wa Marekani.

Wakati huo huo, kijana aliyeuawa na maafisa wa usalama wa katika Ubalozi wa Israel katika mji mkuu wa Jordan, Aman, amezikwa leo. Mamia ya watu wameusindikiza mwili wake, wakitoa matamshi ya kulaani Israel na kuitaka nchi yao isitishe mahusiano ya kibalozi na taifa hilo la kiyahudi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe, dpae

Mhariri:Iddi Ssessanga