Al-Shabaab yadai kuhusika na shambulio mjini Mogadishu
10 Juni 2023Shirika la habari la serikali limeandika kwenye mtandao wao wa Twitter kuwa vikosi vya usalama vinaendesha oparesheni ya kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabab waliohusika na shambulio hilo.
Shirika hilo limeripoti kuwa, "raia wengi" wameokolewa wakiwa hai kutoka hoteli hiyo ya Pearl huku mapigano yakiendelea usiku kucha. Hakuna ripoti zozote za vifo vilivyotokea kutokana na shambulio hilo.
Soma pia: Al-Shabaab washambulia kambi ya Umoja wa Afrika, Somalia
Shambulio katika hoteli ya Pearl ilioko ufukweni mwa bahari lilitokea mapema jana jioni.
Mkurugenzi wa kampuni ya Amin inayomiliki magari ya kubebea wagonjwa Abdikadir Abdirahman amesema wamepokea watu saba waliojeruhiwa katika shambulio hilo.
Kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limesema katika taarifa kuwa, wapiganaji wake wamefanikiwa kuingia katika hoteli ya Pearl ilioko ufuoni mwa bahari na kwamba bado wanaudhibiti.
Kundi la Al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia linajulikana kwa kufanya mashambulizi kwenye hoteli za kifahari na maeneo yenye kutembelewa na watu mashuhuri mjini Mogadishu, aghalabu huanza kwa kufanya shambulio la bomu la kujitoa mhanga.
Hoteli ya Pearl iko karibu na ubalozi wa Uturuki na hutembelewa sana na viongozi na maafisa wakuu wa serikali ya Mogadishu.
Mwishoni mwa mwezi Mei, wapianaji wa Al-Shabab walishambulia kambi ya jeshi la Uganda kilomita 130 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu na kuwaua wanajeshi 54.