Aliyefungwa jela pamoja na Nelson Mandela afariki dunia
22 Julai 2020Mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika kusini Andrew Mlangeni amefariki dunia Jumatano. Mlangeni, ambaye alifungwa jela pamoja na Nelson Mandela mwaka 1964 baada ya kesi ya uhaini, amefariki akiwa na umri wa miaka 95.
Mlangeni, ambaye alitumikia kifungo cha miaka 26 jela na alikuwa mshitakiwa wa sita wa kesi hiyo maarufu ya uhaini kufariki, alilazwa hospitalini kufuatia mtatizo ya kifua, ofisi ya rais wa Afrika kusini imesema katika taarifa.
Rais Cyril Ramaphosa, ambaye alipambana pamoja na Mlangeni kuleta usawa na kufikisha mwisho utawala wa wazungu wachache nchini humo, amemueleza kuwa ni nguzo ya uongozi wa kimaadili na kujali ubinadamu, ambae kifo chake kinafikisha mwisho wa kizazi cha historia na kuweka mustakabali wa nchi hiyo katika mikono ya wale waliobaki.
Mlangeni alizaliwa mwaka 1925 na alijiunga na tawi la vijana wa chama cha ANC mwaka 1951,na baadae alipelekwa nje ya nchi hiyo kwa mafunzo ya kijeshi.