1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International na haki za binadamu

16 Aprili 2008

Amnesty International hairidhiki na ukiukaji haki za binadamu na idadi ya wanaonyongwa China.

https://p.dw.com/p/Dj3a

Amnesty International -shirika linalotetea haki za binadamu ulimwenguni, katika ripoti yake iliotoka jana limesema kuwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini China, unazidi huku michezo ya Olimpik ya Beijing ikikaribia.Ingawa mkuu wa shirika hilo Bibi Irene Khan haridhishwi na ukiukaji wa haki za binadamu nchini China,hakufika umbali wa kuitisha kususiwa kwa michezo ya Beijing.

►◄

" Tumejionea kuzidi unyanyasaji wa haki za binadamu katika kipindi hiki cha kuelekea michezo ya Olimpik.Wakereketwa wameandamwa na kutumiwa kwa kambi za kazi ngumu za mafunzo badala ya kuwaweka watu kizuizini." alisema Bibi Irene Khan.

mkuu huyo wa Amnesty International akizungumza baada ya shirika hilo lenye makao makuu yake mjini London kutoa ripoti kuwa China mwaka uliopita imeongoza katika kupitisha adhabu za vifo duniani.

Adhabu 470 za kunyonga zilitekelezwa nchini China.

Bibi Khan aliekuwa mjini Brussels kukutana na wakuu wa Umoja wa Ulaya aliarifu kumefanyika mabadiliko kidogo huko China.Sasa ni ruhusa kukata rufaa wale waliopitishiwa adhabu ya kifo na hii ya punguza idadi ya wanaonyongwa inayojulikana.

"Tatizo la China , ni kuwa mfumo huo wa kukata rufaa si wazi na hivyo haifahamiki jumla ya watu wanaonyongwa nchini .hivyo ni vigumu kujua iwapo idadi ya wahanga hao yapungua."

Kilicho dhahiri ni kuwa china ingali ikiongoza katika unyongaji kama ilivyokua miaka mingi iliopita-amesema kiongozi huyo wa Amnesty International.

Hatahivyo, Irene Khan haitishi michezo ijayo ya olimpik ya beijing isusiwe kama vilio vinavyosikika kutoka pande nyengine.

"Tunachoitisha ni kuwa wale wenye ushawishi kidogo kama Halmashauri Kuu ya Olimpik Ulimwenguni (IOC) ,makampuni makubwa yaliojitokeza kuwa wahesani wa michezo ya beijing na serikali,watumie ushawishi wao kuifanya China kutimiza ahadi iliotoa ili ichaguliwe wakati ule kuandaa michezo ya olimpik."

Matarajio ya china ya kujenga heba yake ulimwenguni kwa kuupitisha mwenge wa olimpik katika miji 135 mbali mbali katika mabara yote yamepata doa.

Hatua za kwanza za mwenge huo mjini London na Paris ziligubikwa na maandamano ya kupinga mkomoto wa China huko Tibet na hatua ya mwenge huo mjini San Francisco ilibidi kupunguzwa mno na ni watu wachache tu waliouona mwenge ukipita.

Wakati vilio vimepazwa katika miji fulani ya Ulaya kudai alao kususiwe sherehe za ufunguzi za michezo ya Olimpik ya Beijing hapo August 8,mwaka huu,mjumbe wa Ulaya anaehusika na biashara Peter Mandelson alionya jana hadharani kuishinikiza China juu ya swali la Tibet.Alidai kuwa nchi za magharibi zinabidi kushirikiana na dola la China linalokua kiuchumi na sio kulipiga vita.

"Ndio tunaweza na tushikilie juu ya desturi na maadili yetu pamoja na wasi wasi wetu.Lakini pia tusifumbie macho ukweli kwamba itatupasa kushirikiana na China ,kuishi pamoja nayo na kuisaidia ifaulu." alisema Peter Mandelson.

Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani akilihutubia Baraza la ulaya huko Strassbourg hapo jana alizitaka nchi za ulaya kujikosoa linapozuka swali la kukanyagwa haki za binadamu.Alisema kila mmoja atahukum,iwa kwa vitendo vyake.

"Pia ni swali linalohusu desturi na maadili yetu iwapo tunatanguliza haki za binadamu au tunasema maswali ya kiuchumi na haki za binadamu ni maswali yasiofaa kutenganishwa."