Amnesty International yasema UN imeshindwa kuwajibika
24 Mei 2012Katika ripoti yake inayotolewa kila mwaka, shirika hilo limesema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa sasa halina nguvu katika utendaji kazi wake.
Shirika hilo la kutetea haki za binaadam limetaka kutiwe saini kwa makubaliano imara juu ya biashara ya silaha duniani, wakati Umoja wa Mataifa utakapokutana tarehe 2 hadi 27 mwezi Julai mjini New York. Shirika hilo limesema huo utakuwa wakati muwafaka wa kuwapa mtihani viongozi kuamua baina ya kuwa na msimamo madhubuti au kujikita katika faida za kibiashara.
Shirika la Amnesty limetoa mfano wa Umoja wa Kimataifa kushindwa kumaliza umwagikaji damu unaoendelea nchini Syria, likisema kura ya turufu kwa mataifa yanayofanya biashara ya silaha kama Urusi na China, imefanya umoja huo kukosa maana katika kurejesha amani nchini Syria.
Ripoti hiyo pia imezitaja nchi kama India Brazil na Afrika Kusini, kuwa zenye kuridhia ukanadamizaji, kwa sababu ya kukaa kwao kimya kuhusiana na masuala muhimu ya haki za binaadamu.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Katibu mkuu wa shirika la Amnesty Salil Shetty amesema katika karne hii ya 21 Umoja wa Mataifa hauwajibiki. Katibu mkuu huyo ameongeza iwapo Umoja huo hautajirekebisha katika utendaji wake kutakuwa na maswali mengi tu juu ya umuhimu wa kuendelea kuwepo kwake.
Hii ikiwa ni ripoti ya 50 ya shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, limesema mwaka wa 2011 umeonesha mvutano mkubwa katika kutetea haki za binaadamu ambapo waandamanaji wamekuwa wakitoa changamoto kwa serikali, kuwa mabadiliko nchini mwao yanawezekana.
Ripoti hiyo pia imegusia juu ya Myanmar, ambako serikali ya nchi hiyo ilimruhusu mshindi wa tuzo ya Nobel Aung San Suu Kyi kushiriki katika uchaguzi mdogo na hatimaye kuwachia huru wafungwa wengi wa kiasiasa licha ya kuwa mapigano kati ya majeshi ya serikali na makundi ya kikabila, pamoja na hatua za kukamatwa watu upya, ni mambo yanayorudisha nyuma kasi ya mageuzi nchini humo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFPE/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman