Amnesty International yashutumu mateso nchini Nigeria
18 Septemba 2014Wito huo umetolewa katika ripoti mpya ya shirika hilo inayozungumzia kuenea kwa vitendo vya unyanyasaji na utesaji katika mfumo mzima wa sheria za kusimamia uhalifu pamoja na jeshi.Sekione Kitojo anaiangalia kwa undani ripoti hiyo.
Shirika la Amnesty International lenye makao yake mjini London nchini Uingereza limesema katika ripoti yake hiyo iliyopewa jina'' karibu kwenye moto wa jehanamu'' kwamba mateso na vitendo vingine vya kinyama nchini Nigeria vinatokana na ushahidi uliokusanywa kutoka kwa mamia ya wahanga katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Netsanet Belay ambaye ni mtafiti na mwanasheria mkuu katika shirika hilo anasema katika taarifa yake aliyoitowa kando ya ripoti hiyo kwamba uchunguzi huo unakwenda mbali zaidi ya mateso na mauaji yaliyofanywa dhidi ya washukiwa wa kundi la Boko Haram.
Polisi wahusika katika vitendo vya kinyama
Kinachowashtua zaidi hata waangalizi wa haki za binadamu ni kwamba ,uchunguzi uliofanyika umebaini kote nchini Nigeria umefanyika unyama na ukatili dhidi ya wanawake,wanaume na hata watoto,wahusika wakiwa ni maafisa wa serikali wanaotakiwa kisingi kuwalinda wananchi.
Kwahivyo shirika hilo la Amnety International linaitaka serikali ya Nigeria kuchukua hatua za haraka kushughulikia suala hili na hasa kwakua hadi sasa utesaji hauzingatiwi kama kosa la uhalifu nchini humo.
Bunge la nchi hiyo linalazimika kuchukua hatua za haraka na kupitisha sheria ya kukitaja kitendo hicho kuwa uhalifu na hakuna sababu ya hilo kutofanyika linashauri shirika hilo.
Kwa muda mrefu Nigeria imekuwa ikikabiliwa na madai kwamba utesaji unafanyika katika taasisi zake na mnamo mwezi mei mwaka huu shirika hilo la Amnesty International limeitaja nchi hiyo kuwa mojawapo ya miongoni mwa nchi tano duniani ambako utesaji unaotokea kila siku ni suala la kutia wasiwasi.
Hata hivyo kuna ushahidi mdogo kwamba tatizo hilo limeshughulikiwa kikamilifu licha ya Nigeria kutia saini mikataba saba ya kikanda na ya kimataifa inayopinga kitendo hicho huku pia katiba ya nchi hiyo ikikataza kitendo hicho.
Afisa wa polisi wa zamani akiri kufanyika mateso
Mwezi Februari mwaka 2012 aliyekuwa wakati huo mkuu wa polisi ya Nigeria Mohammed Abubakar alikiri kwamba jeshi la polisi lilihusika kuuwa na kuwakamata watu wasiokuwa na hatia.Itakumbukwa kwamba alitamka mbele ya maafisa wakuu kwamba haki haikufanyika,watu wamenyimwa haki,watu wasiokuwa na hatia wametiwa jela,kuteswa na mauaji yamefanyika.Aliongeza kusema vikosi vya kupambana na majambazi vimegeuka kuwa wauwaji wakati maafisa waliozungukwa na rushwa wamepoteza imani ya umma.
Hakuna mtu katika umma wa Nigeria anayeamini kwamba maafisa hao wanaweza kufanya kitu chochote kizuri.Kufuatia ripoti hii mpya Waziri wa habari Laban Maku alikuwa na haya ya kusema.
"Sioni kitu chochote ambacho polisi nchini Nigeria wanafanya ambacho si cha kawaida. Utesaji sio sehemu ya kazi ya polisi na sioni kwamba wanamtesa mtu yeyote. Wanapaswa kupata taarifa. Ninapokuwa mhanga wa kukamatwa na polisi hata ikiwa ni uhalifu mbaya kabisa. Napaswa kuyakabili maswali yao, na katika wakati ambapo nahisi watanichanachana vipande, lakini nadhani wanauliza maswali tu. Wakati polisi wanauliza maswali sijui ni kwanini watu wanaona ni mateso."
Ikumbukwe kwamba Nigeria pia ilianzisha somo la haki za binadamu katika chuo cha mafunzo ya makuruta wapya amesema Mohammed Abubakar mkuu wa zamani wa polisi.
Kwa mujibu wa shirika hilo la Amnesty International kuna aina 12 za mateso yanayofanyika nchini humo ikiwa ni pamoja na watu kupigwa na kufyetuliwa risasi,kuwanyima chakula wanaozuiliwa, kuwakalisha kwenye sehemu zenye vitu vyenye ncha miongoni mwa mengine.
Kiasi madai 500 ya utesaji yameorodheshwa kufuatia mahojiano waliyofanyiwa wahanga,familia zao,mawakali na watetezi wa haki za binadamu tangu mwaka 2007.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef