1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Mwaka 2021 ulijaa usaliti na unafiki wa viongozi

29 Machi 2022

Amnesty International imetoa ripoti yake ya mwaka 2021 ya haki za binaadamu inayoonyesha jumuiya ya kimataifa ilikalia kimya migogoro mipya na ambayo haikuptiwa suluhu na kulaani vikali uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/49AM1
Amnesty International Protest Symbolbild
Picha: Alain Pitton/NurPhoto/picture alliance

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Amnesty International limetoa ripoti yake ya mwaka 2021 kuhusiana na haki za binaadamu ulimwenguni inayoonyesha kwamba jumuiya ya kimataifa ilikalia kimya migogoro mipya na mizozo ambayo haikuweza kupata suluhu huku likilaani vikali uhalifu wa kivita nchini Ukraine wakati mateso dhidi ya raia yakiongezeka tangu Urusi ilipolivamia taifa hilo mwishoni mwa mwezi Februari. 

Soma Zaidi:Ethiopia: Wapiganaji wa Tigray walaumiwa kwa ubakaji 

Ripoti hiyo ya kimataifa ya Amnesty International imekusanya taarifa kuhusu hali ya haki za binaadamu kwenye mataifa 154 ulimwenguni na kuzinduliwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Ripoti hiyo imeyataja mataifa machache ya Afghanistan, Burkina faso, Ethiopia, Israel/Palestina, Libya, Myanmar na Yemen ambako mivutano ilisababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za kimataifa za binaadamu pamoja na sheria ya kiutu na kusisitiza kwamba mataifa makubwa ulimwenguni hayakuchukua hatua ya kuwawajibisha waliofanya ukiukwaji huo.

Ukraine Protest in Thailand
Shirika la Amnesty limelaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine hali inayoongeza mateso kwa raiaPicha: Varuth Pongsapipatt/SOPA/ZUMA/picture alliance

Amnesty lalaani vikali uhalifu wa kivita, Ukraine.

Aidha ripoti hiyo iliyochapishwa hii leo imelaani vikali uhalifu wa kivita nchini Ukraine wakati idadi ya raia wanaoteseka ikiongezeka tangu Urusi ilipoivamia Ukraine na kuyafananisha mazingira hayo kama yaliyojitokeza kwenye vita vya Syria.

Katibu mkuu wa Amnesty Agnes Callamard ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kile kinachotokea Ukraine ni marudio tu ya kile kilichoshuhudiwa Syria huku akiishutumu Urusi kwa kuzigeuza njia salama la raia kama "mitego ya kifo" na kusema ni kama alichokifanya Syria.

Mkurugenzi wa Amnesty mashariki mwa Ulaya Marie Struther aliunga mkono hilo akiwa mjini Paris akisema watafiti nchini Ukraine wamerekodi matumizi ya mbinu sawa na zilizotumiwa Syria na Chechnya ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya raia na matumizi ya silaha yaliyopigwa marufuku chini ya sheria ya kimataifa.

Aidha, Callmard amekosoa namna ambavyo baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilivyoshindwa kuchukua hatua vya kutosha dhidi ya ukatili uliofanywa katika maeneo kama Myanmar, Afghanistan na Syria na kuonya kusitokee upendeleo wakati wa kulishughulikia suala la Urusi.

Pfizer-BioNTech Impfstoff gegen das Corona-Virus
Amnesty imekosoa namna mataifa tajiri yalivyojilimbikizia chanjo, huku mataifa masikini yakihaha kupata chanjo hizo.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Mataifa makubwa yakosolewa kuhusiana na kukosekana kwa usawa wa chanjo ya COVID.

Kundi hilo aidha, limeyakosoa mataifa ya magharibi kuhusu namna ilivyoshughulikia janga la virusi vya corona nje ya mipaka yao likisema wameshirikiana na wazalishaji wakubwa wa chanjo na kusababisha kukosekana kwa usawa wa mgao wa chanjo kati ya mataifa tajiri na masikini na hususan ya Afrika. Kulingana na ripoti hiyo mataifa ya kipato cha juu yalijilimbikizia mamilioni ya dozi za chanjo na kuwa na uwezo wa kuwachanja watu wao wote hata zaidi ya mara tano.

Soma Zaidi: Janga la Covid-19 limepora haki za wanawake na wasichana

Aidha ripoti hiyo, imekosoa mazingira ya wafanyakazi wa kigeni wanaoandaa michuano ya kombe la dunia nchini Qatar huku ikipinga kuongezeka kwa vizuizi juu ya uhuru wa kujieleza kwenye mataifa mengi ulimwenguni.

Ripoti hiyo ya Amnesty International inahitimisha kwamba mwaka 2021 kwa kiasi kikubwa ulijaa hadithi za usaliti na unafiki na hasa kutoka kwenye mamlaka ikiangazia zaidi suala la kukosekana kwa usawa wa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Mashirika: AFPE/APE