Amnesty: Vikosi vya usalama Tunisia vilihusika na utesaji
13 Februari 2017Ripoti ya shirika la Amnesty International iliyochapishwa leo (13.02.2017), inaelezea jinsi vitendo vya kikatili vinavyofanywa na vikosi vya usalama, vinavyokiuka haki za binaadamu. Mkurugenzi wa shirika hilo katika ukanda wa Afrika Kaskazini, Heba Morayef amesema vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia mbinu hizo kwa mujibu wa sheria ya hali ya hatari iliyowekwa na serikali ya Tunisia kwa lengo la kupambana na ugaidi, ingawa anasema zinahatarisha mchakato wa mageuzi katika taifa hilo.
Ripoti hiyo iliyopewa jina ''Mwisho wa hofu: mateso chini ya sheria ya hali ya hatari Tunisia,'', inaelezea kwa undani visa 23 vya utesaji na ukatili vilivyofanywa na polisi, walinzi wa taifa na brigedi ya kupambana na ugaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Morayef anasema hali ya kutojali kutoshtakiwa imechochea utamaduni wa ukatili na ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa na vikosi vya usalama.
Waathirika walionukuliwa katika ripoti hiyo, wamesema walipigwa kikatili kwa kutumia fimbo na mipira. Pia waliwekwa katika mazingira magumu ikiwemo kulazimishwa kusimama kwa muda mrefu, kuteswa kwa kutumia umeme, kuzuiwa kulala na wakati mwingine walimwagiwa maji ya baridi.
Mhanga mmoja ameiambia Amnesty International kwamba alipigwa miguu yake hadi kucha za miguuni zikatoka zenyewe, huku mwingine akielezea jinsi alivyolawitiwa kwa kutumia fimbo akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Utesaji huo pia ulihusisha kuwaweka kizuizini na kuwazuia kusafiri watuhumiwa wa ugaidi, lakini pia familia zao zilibughudhiwa na kunyanyaswa.
Watu 5,000 wapigwa marufuku kusafiri
Shirika la Amnesty International limesema kuwa viongozi wa Tunisia wameweka marufuku ya kusafiri kwa kiasi ya watu 5,000 na imezuwia kutembea kwa wengine kadhaa kwa ajili ya kuwazuia wananchi kujiunga na makundi ya jihadi nchi za nje.
Morayef anasema hakuna shaka kwamba viongozi wana jukumu la kupambana na vitisho vya usalama na kuwalinda wananchi wake na mashambulizi yanayosababisha mauaji, lakini wafanye hivyo kwa kuheshimu haki za binaadamu ambazo zimewekwa na katiba ya Tunisia pamoja na sheria ya kimataifa.
Ben Emmerson, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binaadamu na kupambana na ugaidi, alitumia siku tatno nchini Tunisia mwanzoni mwa mwaka huu kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika kuimarisha haki za binaadamu.
Mwishoni mwa ziara yake, Emmerson alipongeza juhudi za Tunisia za kupambana na ugaidi, lakini akasema mapambano hayo yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia haki za binaadamu ili kutumika kama mfano wa kuigwa ndani na nje ya ukanda huo.
Tangu kutokea mapinduzi ya Tunisia ya mwaka 2011 yaliyochochea mapinduzi ya msimu wa machipuko katika mataifa ya Kiarabu, Tunisia imekabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi ambayo yamewaua zaidi ya wanajeshi na askari polisi 100, kiasi ya raia 20 pamoja na watalii 59 wa kigeni.
Hali hiyo ilisababisha maafisa kuchukua hatua kadhaa za kiusalama na tunisia imekuwa chini ya utawala wa hali ya hatari tangu Novemba 2015, lilipotokea shambulizi na kuwaua walinzi 12 wa kikosi cha ulinzi wa rais.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf