1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yalaani kufungwa wanahabari Burundi

31 Januari 2020

Amnesty International na waandishi wa habari wasio mipaka wamekosoa uamuzi wa mahakama ya Burundi kuwafunga waandishi wanne wa habari miaka miwili na nusu jela kwa hatia kuhatarisha usalama wa nchi.

https://p.dw.com/p/3X51w
Archivbild - Burundi's President Pierre Nkurunziza
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

"Kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwa Agnes Ndirubusa, Christine Kamikazi, Egide Harerimana na Terence Mpozenzi kwa mashitaka ya kubambikiziwa kunaashiria siku ya huzuni kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa wanahabari nchini Burundi," alisema Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki, Seif Magango, akizitolea wito mamlaka za Burundi kuifuta hukumu na adhabu hiyo na kuwaachilia waandishi hao haraka na bila masharti. 

Amnesty International ilisema waandishi wa habari wanapaswa kuachiwa kufanya kazi zao kwa uhuru hasa kwenye kipindi ambapo taifa hilo la Afrika Mashariki linaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Mei 2020.

Shirika la Waandishi wa Habari Bila Mipaka, ambalo linaiweka Burundi kwenye nafasi ya chini ya 159 kwenye orodha ya uhuru wa habari duniani, linasema waandishi hao walikuwa wakifanya kazi zao tu.

Wakili wa waandishi hao, Clement Retirakiza, amesema kuwa hukumu hiyo haikuwa ya haki na kwamba ataikatia rufaa mahakamani. Dereva wa waandishi hao, Adolphe Masabarakiza, ameachiwa huru.

Mwanzilishi wa shirika la habari la Iwacu, Antoine Kaburahe, anayeishi uhamishoni nchini Ubelgiji, naye pia alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema kuwa shirika lake litaikatia rufaa hukumu hiyo.

Antoine Kaburahe
Mwanzilishi wa Iwacu, Antione KaburahePicha: DW/F. Muvunyi

Waandishi hao wa habari walikuwa wakiifanyia kazi Iwacu, moja ya vyombo vichache huru vya habari nchini Burundi, walipokamatwa tarehe 22 Oktoba mwaka jana na kushitakiwa kwa kuhatarisha usalama wa nchi. 

Faini ya dola 535 

Mmoja wa watu waliokuwapo mahakamani mjini Bujumbura wakati kesi hiyo ikitolewa hukumu, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba walishitushwa na hukumu hiyo, mbali na kifungo cha miaka miwili unusu jela, imewaamuru waandishi hao pia kulipa faini ya faranga milioni moja za Burundi, sawa na dola 535 za Kimarekani, kila mmoja. 

Awali upande wa mashitaka uliiomba mahakama itowe hukumu ya miaka 15 jela, wakitumia ushahidi wa mazungumzo ya WhatsApp katika ya mmoja wa waandishi hao na mwenzao aliyeko nje ya nchi, ambao unasomeka: "Tunaelekea Bubanza...kuwasaidia waasi." Baadaye upande huo wa mashitaka ulipendekeza tena kifungo cha miaka 20 jela. 

Polisi inasema waasi 14 wa kundi la RED-Tabara lililo kwenye mpaka wa Burundi na Kongo waliuawa katika siku ambayo waandishi hao walikamatwa. Waasi hao kwa upande wao wanasema waliwauwa maafisa kadhaa wa usalama kwenye makabiliano hayo.

Katika miaka michache ya hivi karibuni, Rais Pierre Nkurunziza amekuwa akiyaandama makundi ya haki za binaadamu kwa kujiondowa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, kuwafukuza wachunguzi wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, kuyafungia makundi ya haki za binaadamu na kuwalazimisha waandishi wa habari kukimbilia uhamishoni.