Amnesty yalaani utesaji wa mahabusu Syria
18 Agosti 2016Shirika hilo la Amnesty International limesema wafungwa 17,723 wamepoteza maisha wakiwa chini ya ulinzi wa serikali, kati ya mwaka 2011 pale machafuko yalipozuka nchini humo kupinga utawala wa Rais Bashar al-Asaad , hadi mwaka 2015. Kwa wastani kila mwezi kunarikodiwa zaidi ya vifo vya watu 300.
Ukandamizaji wa serikali dhidi ya upinzani pamoja na kuzuka kwa makundi ya wanamgambo wanaopambana kwa kutumia silaha, kulipelekea kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya raia 250,000, nusu ya idadi nzima ya watu wa nchi hiyo kupoteza makaazi yao na wengine milioni 4 laki 8 kugeuka kuwa wakimbizi. Ingawa shirika la Amnesty International linaamini kuwa maelfu ya watu wamewekwa vizuizini kwa nguvu katika vituo mbali mbali hadi kusahaulika, idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi ya inayoaminika.
Philip Luther, Mkurugenzi wa Shirika la Amnesty International kwa upande wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amepigia kelele ukamatwaji wa watu kiholela na mateso yaliyokithiri dhidi ya wafungwa nchini Syria.
"Kinachoendelea chini kwa chini nchini Syria ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu, mateso, ueneaji wa ukiukwaji wa haki za binaadamu, na maelfu ya watu waliokufa chini ya ulinzi wa serikali ya Syria tokea mwaka 2011."
Serikali ya Syria yatumia mateso ya kinyama
Kutokana na mahojiano yaliyofanwa na shirika hilo na wafungwa 65 waliowahi kuteswa katika vituo vya aina hiyo, ripoti hiyo inaeleeza unyanyasaji katika vituo vya usalama vinavyolindwa na mashirika ya ujasusi ya Syria pamoja na katika jela ya kijeshi ya Saidnaya iliyo karibu na mji mkuu wa Damascus. Wengi wao wameelezea kushuhudia mauwaji mara kadhaa wakiwa wafungwa katika magereza hayo.
Ripoti hiyo inaeleza baadhi ya mateso yanayotumika kuwaadhibu wafungwa katika vituo hivyo ni pamoja na kutumia mshituko wa umeme, ubakaji na ukatili mwengine wa kijinsia, kuwanyofoa wafungwa kucha za vidole vya mikono na miguu, kuwachoma kwa kutumia maji ya moto pamoja na kuwachoma kwa sigereti.
Samer aliwahi kuwa mahabusu katika vituo hivyo na anasema na hapa ninamnukuu, "wafungwa wanawekwa katika hali ya kinyama, na wanakuvunja ubinaadamu wako. Sijawahi kuona mtu yoyote akifariki lakini niliiona damu, na ilikuwa nyingi ikitiririka kama mto." Kulingana na Amnesty Samer alikamatwa kwa nguvu wakati alipokuwa akisafirisha misaada ya kiutu.
Kwa mujibu wa Amnesty International mtu yoyote yule anayejaribu kuipinga serikali yuko katika hatari ya kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini, kuteswa, kupotea asijulikane alipo na hatimaye kuuawa kabisa.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/dw
Mhariri: Iddi Ssessanga