Amnesty yalaumu Uturuki kuruhusu ukiukwaji wa haki Afrin
2 Agosti 2018Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International, limeyashutumu majeshi ya Uturuki kwa kuyaruhusu makundi yenye silaha ya Syria kufanya ukiukaji mkubwa wa binadamu kaskazini mwa eneo la Afrin. Shirika hilo limeitaka Uturuki kusitisha mara moja ukiukaji wa haki.
Wanajeshi wa Uturuki wanaoshirikiana na waasi wa Syria, walichukua udhibiti wa Afrin mapema mwaka huu, baada ya operesheni ya kijeshi ambayo iliwaondoa wanamgambo wa Kikurdi ambao ni washirika wa Marekani, lakini ambao Uturuki inawachukulia kama kundi la kigaidi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema tangu Uturuki na washirika wake kuchukua udhibiti wa Afrin, wakaazi wa eneo hilo wamekumbwa na visa kadhaa vya ukiukaji wa haki zao, huku wanajeshi wenye silaha wa Uturuki wakifumba macho.
Majeshi ya Uturuki yajitia upofu?
Shirika hili limeongeza kuwa ukiukaji huo ni pamoja na watu kuwekwa kizuizini bila sababu, watu kutoweka kwa kulazimishwa, mali kuchukuliwa kwa nguvu pamoja na wizi. Lakini majeshi ya Uturuki yamejitia upofu kuhusu visa hivyo.
Lynn Maalouf ambaye ni mkurugenzi wa utafiti wa Amnesty International Mashariki ya Kati, amesema makundi yenye silaha ya Syria yameendelea kukiuka haki za raia, bila ya matendo yao kuchunguzwa au kuwajibishwa na majeshi ya Uturuki.”
Maalouf amehoji kuwa Uturuki ina wajibu kuzingatia masilahi ya raia pamoja na kuhakikisha kuna usalama na sheria, kwani ‘inashikilia madaraka' katika eneo la Afrin.
Amesisitiza kuwa ni lazima Uturuki isitishe mara moja ukiukaji wa haki unaofanywa na makundi yenye silaha yanayounga mkono Uturuki, na ichukue hatua dhidi ya watakaokutikana na hatia na ijitolee kuwasaidia wakaazi wa Afrin kujenga upya maisha yao.
Masomo ya watoto yatatitizwa
Amnesty International imeongeza kuwa, baadhi ya makundi ya Syria pamoja na majeshi ya Uturuki yamechukua shule, hali ambayo imevuruga masomo ya maelfu ya watoto.
Amnesty imesema wakaazi wameiambia kuwa chuo kikuu cha Afrin kimefungwa kabisa baada ya kuharibiwa na mali kuibwa, na kwamba ni shule moja pekee ambayo imesalia katika mji wa Afrin.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema, lilipouliza serikali ya Uturuki kutoa kauli yake, serikali hiyo iliibua swali kuhusu sifa ya Amnesty International ya kutoegemea upande wowote, kutokana na shirika hilo kurejelea eneo hilo kuwa lililotawaliwa na wapiganaji wa Kikurdi.
PKK imeorodheshwa kama kundi la kigaidi
Uturuki inasema kuwa kundi la wapiganaji wa Kikurdi (YPG) ambalo ililitimua kutoka Afrin, ni kikosi kilichoibuka kutoka kwa Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi (PKK) ambacho kimekuwa kikiendeleza mapigano nchini Uturuki tangu 1984.
Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeliorodhesha kundi la PKK kuwa la kigaidi
Katika kisa cha mwanamke mmoja, mjomba wake ametoweka tangu kundi la watu waliokuwa na silaha kumchukua nyumbani kwake, baada ya kurudi kijijini kwao miezi mitatu iliyopita.
Hawakumueleza mke wake, ni wapi walimpeleka. Mwanamke huyo mzee aliielezea Amnesty International huku akikana kuwa mtu huyo hakuwa mkuu wa kamati ya kijijini chenye mafungamano na kundi la YPG.
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Josephat Charo