Haki za binadamu, majivuno ya wanaume na #MeToo
10 Desemba 2018Asilimia 49.5 ya watu wote duniani ni wanawake. Licha ya hilo, ni asilimia 17 tu ya wakuu wa nchi na serikali ndiyo wanawake, na asilimia 23 ya wabunge ndiyo wanawake. Takwimu hizi kutoka ripoti mpya ya Amnesty International iliotangazwa leo zinaonyesha umbali gani tunahitaji bado kwenda kufanikisha usawa wa kijinsia.
Katibu mkuu wa Amnesty International Kumi Naidoo, alisema haki za wanawake daima zimewekwa chini ya haki na uhuru mwingine, na kuzilaani serikali zisizojali masuala haya na kutofanya vya kutosha kulinda haki za nusu ya wakaazi wa dunia. Shirika hilo la haki za binadamu lilibanisha hasa, ongezeko la lilichokitaja kuwa watu makatili miongoni mwa viongozi wa serikali, wanaowakilisha sera za chuki dhidi ya wanawake na wageni.
Mwaka wa wanawake
Hata hivyo Naidoo ameutaja mwaka huu wa 2018 kuwa mwaka wa upinzani wa wanawake. Katika utangulizi wake wa ripoti hii, anakumbushia maandamano yaliotika dunia ya kampeni ya #MeToo ya kupinga unyanyasaji wa kingono pamoja na mapambano ya wanawake kupigania haki nchini Nigeria kufuatia mashambulizi ya kundi la itikadi kali la Boko Haram na wanajeshi.
Katika kanda ya Amerika Kusini, vuguvugu la wanawake lisilojulikana ukubwa wake, liliignia mitaani chini ya kaulimbiu ya "Ni una menos" -"hakuna kidogo". Ametaja baadhi ya mataifa ambako hali ya wanawake imeboreka, kama vile Ireland ambako haki ya kutoa mimba ililegezwa kupitia kura ya maoni, au Saudi Arabia ambako wanawake waliruhusiwa kuendesha magari kuanzia msimu wa kiangazi mwaka huu.
Hata hivyo amesema mafanikio hayo ya kiasi hayapaswi kuficha madai ya muda mrefu: Kwa mujibu wa Amnesty, asilimia 40 ya wanawake waliofikia umri wa kuza watoto katika mataifa ambako utoaji mimba unadhibitiwa, na karibu wanawake milioni 225 hawapati kingamimba za kisasa. Na pia pengo la malipo kati ya wanawake na wanaume bado linasalia kuwa asilimia 23.
Kwa mwaka 2019, Amnesty International inataka hatimaye kufunguliwa ukurasa mpya. Kuliko wakati wowote ule, tunapaswa kusimama pamoja na mavuvugu ya wanawake, kuzifanya sauti za wanawake zisikike katika utofauti wao wote, na kupigania utambuzi wa haki zote, alisema Katibu mkuu Naidoo.
Hali ya mkwamo kwa wakimbizi
Katika ripoti hiyo ya kurasa 52, shirika hilo la haki za binadamu pia linachambua hali ya wakimbizi duniani inayozidi kuzorota. Kulingana na shirika la wakimbizi duniani UNHCR, wakimbizi 75,200 ndiyo walipatiwa makaazi mapya mwaka uliopita, hii ikiwa ni asilimia 54 chini ya idadi ya mwaka 2016 (163,200). Kwa mujibu wa UNHCR, nafasi milioni 1.2 zinahitajika kila mwaka.
Amnesty International haiamini kuwa mktaba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi, ambao kwa sasa uko katika ngazi ya mashauriano, utabadili pakubwa hali hii. Ripoti hiyo inautaja mkataba huo kuwa ni "mpango wa kufedhehesha wa kukwepa majukumu".
Kwa Warohigya au vijana wa Kisomali waliozaliwa katika kambi za wakimbizi nchini Kenya, au wakimbizi walioko kwenye kambi haramu visiwani Nauru, hautabadili chochote.
Mkataba kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, ambao chini yake Uturuki inawahifadhi wakimbizi kwa kutumia fedha za Umoja wa Ulaya, pia unatazamwa na wanaharakati wa haki za binadamu kama "nkuta ya rejea juu ya namna ya kukwepa uwajibikaji."
Kuimarika kwa jamii za Kiafrika
Barani Afrika, Amnesty International inashuhudia mapambano ya tatu ambayo jamii zinapaswa kukabiliana nayo: Kwa kuwa sasa wamepata uhuru wao kutoka kwa watawala wa kikoloni na baadhi ya mataifa yameondokana na tawala za mabavu, ni suala la "kuthaminisha wajibu wa sheria za kitaifa na haki za binadamu kuliko karatasi ambako zimeandikwa."
Serikali nchini Misri kwa mfano, inakosolewa, na wakosoaji wanafungwa gerezani. Shirika hilo linasifu hatua zilizopigwa nchini Ethiopia, ambayo inazidi kufanya maboresha chini ya uongozi wa waziri mkuu mpya Abiy Ahmed. Hatan hivyo, ripoti hiyo pia inazungumzia vizuwizi kama vile ukamataji hovyo wa vijana 3,000 mwezi Septemba, kwa madai ya kuongezeka kwa uhalifu. Habari nzuri zaidi kutoka Afrika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni "kuendelea kwa ujasiri usio wa kawaida unaooneshwa na watu wa kawaida barani humo".
Vyanzo kadhaa vya moto barani Asia
Amnesty inaelezea kambi za mateso katika mkoa wa China wenye utawala wake wa ndani wa Xinjiang, ambako watu takribani milioni moja wa jamii ya Uighur na watu wa jamii nyingine za wachache watatiwa kasumba, kama "moja ya matukio ya kusikitisha zaidi ya mwaka ". Ripoti hiyo pia inamulika kwa namna ya kipekee, kuhusu hali nchini Myanmar, ambako watu 720, 000 wa jamii ya Waislam wa Rohingya, walikimbia na kuingia nchi jirani ya Bangladesh.
Katika kanda ya mashariki ya kati, Amnesty inalamikia hasa vita nchini Yemen, ambamo raia 17,000 wamejeruhiwa au kuuawa mpaka sasa. Sakata la mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi, limevutia nadhari kuhusu hali nchini Saudi Arabia, ambako leseni za udereva kwa wanawake ni jambo la tahfifu zaidi kuliko utoaji wa haki zaidi za msingi za kiraia. Machafuko yanayoendelea katika ukanda wa Gaza kati ya jeshi la Israel na waandamanaji wa Kipalestina ambapo zaidi ya Wapalestina 150 wameuawa zimemulikwa pia.
Nyakati za dhoruba Ulaya
Kuongezeka kwa hali ya kukosa uvumilivu, chuki na ubaguzi katika muktadha wa kupungua kwa nafasi ya jamii ya kiraia kunapanua pengo katika mfumo wa kijamii wa kanda," imeandika Amnesty kuhusu Ulaya. "Sera ya hofu inawatenganisha watu, huku viongozi wakitumia maneno ya sumu kwa kuyalaumu makundi ya watu kwa matatizo ya kijamii na kiuchumi. Inatolea mfano wa nchini Uturuki, ambako watumishi 130,000 wa umma wamefututwa kazi hovyo.
Uhuru na hadhi ya mahakama ya sheria ya Ulaya pia vinazidi kukabiliwa na kitisho. Baadhi ya mataifa yalikataa kutekeleza hukumu zinazofungamanisha. Lakini shirika hilo pia linathibitisha juu ya upinzani wa kiraia unaozidi: "Vuguvugu pana la watu wa kawaida wenye mapenzi makubwa wanatagaza haki na usawa".
Mashambulizi Amerika
Katika msimu wa mapukutiko, mtu angeweza kuamini kwa muda mfupi kwamba vuguvugu la #MeToo halijawahi kuwepo nchini Marekani: Donald Trump alifanikisha kuidhinishwa mteule wake wa mahakama ya juu, Brett Kavanaugh, hata baada ya profesa kutoa ushahidi mbele ya baraza la Seneti kwamba alitaka kumbaka wakati wa ujana wake, na licha ya maelfu ya wanawake kuandamana dhidi ya Kavanaugh. Ripoti pia inakosoa hatua ya kutenganishwa kwa mamia ya watoto na familia zao baada ya kuvuka mpaka kinyume na sheria.
Vinginevyo, ripoti inajikita zaidi kwenye mataifa ya Amerika ya Kati na Kusini, ambako raia wananyanyaswa mara kwa mara na watawala. Amnesty inalalamikia namna, kwa mfano, mahakama za Colombia zinavyotumiwa vibaya kunyamazisha watetezi wa haki za binadamu. Katika taifa hilo, mwanaharakati huuawa kila baada ya siku tatu kwa wastani. Lakini kuna matumaini pia, kama vile kukamatwa kwa watu tisa nchini Honduras, ambao wanasemekana kuhusika na kifo cha mwanaharakati.
Mwandishi: David Ehl
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Bruce Amani