1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola hawana hofu kupambana na Algeria

15 Januari 2024

Katika mojawapo ya mechi za Jumatatu Algeria ambao wanaingia uwanjani kwa mara ya kwanza kushiriki mechi yao ya kwanza katika kundi D dhidi ya Angola, wamelishinda taji la AFCON mara mbili.

https://p.dw.com/p/4bGN6
Mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 - Msumbiji v Algeria
Nahodha wa Algeria Riyadh MahrezPicha: BackpagePix/empics/picture alliance

Katika mashindano yaliyopita yaliyokuwa huko Cameroon, Algeria waliyaaga mashindano mapema katika duru ya makundi ila safari hii matumaini yako juu kama anavyoeleza nahodha wao Riyadh Mahrez.

"Tumejiandaa kama zilivyojiandaa timu zote katika mashindano haya. Kama kocha wetu alivyosema, tuna malengo kama timu zengine ila nafikiri cha muhimu ni sisi kuanza mechi hii kwa lengo la kuanza mashindano vyema na baada ya hapo tutaona kitakachotokea," alisema Mahrez.

Ama upande wa wapinzani wa Algeria, Angola, wao hawajawahi kuyashinda mashindano haya na matokeo mazuri ambayo wamewahi kuyapata ilikuwa ni katika mashindano ya kufuatana ya mwaka 2008 huko Ghana na 2010 walipokuwa waandalizi ambapo walifika hatua ya robo fainali.

Lakini nahodha wao Alfredo Kulembe Ribeiro anasema kucheza dhidi ya timu bora ni motisha kwao.

"Bila shaka tunataka kucheza dhidi ya timu bora na Algeria ni moja ya timu bora Afrika na duniani. Huo ni motisha kwetu lakini pia tunataka kushiriki mashindano haya na kuwathibitishia watu kile tunachoweza kukukifanya. Wengi hawatufahamu vyema na hilo ni jambo linalotupa motisha. Tunaujua uwezo wetu, tunayo historia yetu na tunataka kuendelea kuweka historia," alisema Ribeiro.

Chanzo: Reuters/AP/AFP