Angola: Tajiri wa mafuta mwenye sura nyingi
Angola inashika nafasi ya pili barani Afrika katika nchi zinazochimba mafuta kwa wingi. Hivi karibuni Angola inatarajia pia kuuza gesi. Wakati uchumi wa nchi hiyo ukikuwa, tofauti katika jamii zinaongezeka.
Maisha ya kila siku katika matope
Zaidi ya watu 400,000 wanaishi katika eneo lenye kilometa 40 za mraba kwenye kitongoji cha Cazenga, magharibi mwa mji mkuu Luanda. Wengi wao ni maskini. Hakuna barabara za lami na umeme unakatika mara nyingi. Wanasiasa wengi wa chama tawala cha MPLA wanatokea katika eneo hili. Hata hivyo, hakuna aliyeanzisha mradi wa maendeleo au miundombinu kwa ajili ya Cazenga.
Chama kimoja, rais mmoja
["MPLA ni chama cha rais! Tangu kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe amejaribu kuachia madaraka lakini raia wanataka abaki. Hivyo anaendelea." Euricleurival Vasco mwenye miaka 27 anaelezea aliyempigia kura katika uchaguzi wa 2012. Wakosoaji wanasema kuwa hadi sasa rais José Eduardo dos Santos hajatimiza hata ahadi moja aliyoitoa katika kampeni, kama vile ahadi ya kuleta maji na umeme.
Hakuna ajira kwa raia
Takriban asilimia 40 ya wananchi wa Angola wanaishi kwa kutegemea chini ya dola moja kwa siku. Wengi wao walitarajia kupata ajira na maisha bora zaidi kutokana na kukua kwa biashara ya mafuta. Lakini sasa wanapata fedha kidogo tu za kutosha kununulia chakula au wanategemea biashara haramu kama wanawake hawa wanaouza biskuti.
Fahari ya Luanda
Mpaka sasa faida za mauzo ya mafuta zimeufikia tu mji mkuu Luanda. Mji huo tayari ni mmoja wa miji yenye gharama kubwa kabisa ya kuishi duniani. Anayetaka kukodi nyumba ni lazima alipe dola 5,000 na zaidi. Utajiri wa mji huo unaonekana dhahiri kabisa katika Baía de Luanda yaani ghuba ya Luanda. Kila mahali zinajengwa nyumba mpya za ghorofa.
Bunge la Angola
Jengo jipya la bunge linajengwa karibu na Baía de Luanda. Viti 175 kati ya 220 vinakaliwa na chama tawala cha MPLA. Chama kikuu cha upinzani, UNITA, kina wabunge 32. Kila wakati chama hicho kinalalamika juu ya nafasi ndogo inayopewa na chama tawala.
Mwanamume wa Angola mwenye nguvu
Kwa mujibu wa wakosoaji, rais José Eduardo Dos Santos, anayeonekana hapa katika bango la kampeni, anatawala kila kitu – serikali, bunge na vyombo vya sheria. Dos Santos ameiongoza Angola kwa miaka 33 sasa. Tarehe 20 Septemba 1979, katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, alichukua nafasi ya rais Agostinho Neto kama rais na mwenyekiti wa chama.
Kujenga upya kwa muda mfupi kabisa?
Miaka kumi baada ya vita kumalizika (1975-2002) bado kuna mabomu ya kutegwa ardhini katika maeneo ya vijijini, kama hapa karibu na mji wa Soyo uliopo kaskazini mwa nchi. Angalau sasa kuna barabara zinazounganisha miji midogo midogo. Mwaka 2002 ilikuwa vigumu sana kusafiri kutoka upande mmoja wa nchi hadi mwingine kwa kutumia gari.
Utajiri chini ya ardhi
Mbali na utajiri mkubwa wa mafuta, Angola pia ina machimbo ya gesi katika pwani yake. Mtambo wa kwanza wa kuchimba gesi ya kimiminika umejengwa katika mji wa Soyo lakini hadi sasa upo katika hatua za majaribio. Mtambo huo unatarajiwa kuzalisha tani milioni 5,2 za gesi kwa mwaka.
Njia mbadala baada ya mafuta kuisha
Angola inategemea mauzo ya mafuta kwa kiasi kikubwa. Oktoba 2012 serikali ilianzisha mfuko wa kuwekeza ndani na nje ya nchi ili kujizatiti kutokana na athari za kuyumba kwa bei na akiba ya mafuta. Hata hivyo, kiasi cha mafuta kilichopo kinatarajiwa kutosha kwa miaka 20 hadi 30 tu ijayo. Wataalamu wanaona uwekezaji katika kilimo kama njia mbadala.
Wawekezaji kutoka nje
Ni kawaida kuona mabango ya matangazo ya wawekezaji wa kichina Angola. Wachina wanaunda kundi kubwa zaidi la wageni wakifuatiwa na Wareno na Wabrazil. Kwa kuwa Brazil haiwezi kushindana na Wachina katika uwekezaji, imeamua kujikita zaidi katika kutoa mafunzo ya teknolojia kwa raia wa Angola.
Maisha katika banda la mabati
Mwalimu Fernando Pinto Ndondi anaitaka serikali ya Angola iwekeze kwa binaadamu na si katika ujenzi wa barabara za lami. Mshahara wake ni dola 300 kwa mwezi, fedha anazozitegemea kuwalisha watoto wake watano. Ndondi anaishi katika kijiji cha Viana karibu na Luanda. Kwa sasa hana nyumba kwa sababu nyumba yake ilibomolewa katika harakati za kujenga barabara.
Pesa inakwenda wapi?
Angola inashika nafasi ya 168 kwenye orodha ya nchi 182 iliyotengenezwa na shirika la kupambana na rushwa ulimwenguni, Transparency International. Dola bilioni 32 zilizopatikana kwenye mauzo ya mafuta ya shirika la serikali Sonagol kati ya mwaka 2007 na 2010 zimekwenda wapi? Shirika linasema kwamba fedha imetumika kwenye miradi ya miundombinu. Hata hivyo haifahamiki ni miradi gani hasa.