ANKARA:Wahamiaji 3 wakiafrika wazama Uturuki
24 Agosti 2007Wahamiaji haramu watatu wa Kiafrika wamezama karibu na pwani ya magharibi mwa Uturuki pale mtumbwi wao ulipojaa maji.Mtumbwi huo ulikuwa unaelekea visiwa vya Ugiriki kwa mujibu wa shirika la habari la Ugiriki la Anatolia.
Maafisa wa polisi wa pwani walipata miili hiyo na mtumbwi wao wa plastiki karibu na mkahawa wa Cesme unaopakana na kisiwa cha Chios cha Ugiriki. Wahamijai hao wanatokea nchi za Gambia,Mauritani na Rwanda.
Nchi ya Uturuki iko katika njia muhimu ya kusafirisha wahamiaji haramu kimagendo kutoka bara Asia hadi Ulaya na matukio kama hayo ni ya kawaida.
Wahamiaji wengi haramu hujaribu kuingia Ugiriki kwa barabara kisha kujaribu kuvuka bahari ili kuingia Italia.
Wiki jana boti moja lililokuwa na wahamiaji 50 lilizama katika eneo hilohilo na watu 6 kupoteza maisha yao wengi wao wakitokea Afganistan na Pakistan.