Annan akutana na Assad
10 Machi 2012Mazungumzo ya Annan mjini Damascus yanakuja siku moja baada ya wanaharakati kusema kuwa majeshi ya utawala wa rais Assad yamewauwa watu 68 wakati yakijaribu kupanua udhibiti wao dhidi ya mji wenye uasi wa Homs na kuzima upinzani wa kundi la watu wenye silaha katika jimbo la kaskazini la Idlib.
Arab League kukutana
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya Kiarabu pia wanatarajiwa kuwa na mazungumzo mjini Cairo na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov. Urusi na China zilipiga kura ya veto dhidi ya mswada wa umoja wa mataifa mwezi uliopita ambao ungeunga mkono mpango wa umoja wa mataifa ya Kiarabu unaotaka Assad kujiuzulu.
Wanaharakati wamesema kuwa makombora yaliyofyatuliwa kutoka katika vifaru pamoja na mabomu kadha yameanguka katika wilaya zinazoshikiliwa na wapinzani katika mji wa Homs, na kuuwa watu 20, ambapo 24 wameuwawa katika jimbo jirani la Idlib na vifo zaidi vimeripotiwa kwingineko.
Vifaru 30 viliingia katika kitongoji chetu asubuhi ya leo na wanafyatua makombora katika nyumba, amesema Karam Abu rabea, mkaazi wa kitongoji cha Karm al-Zeitoun katika mji wa Homs.
Urusi yatakiwa kusaidia
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Rodham Clinton siku ya Ijumaa amesema kuwa ana matumaini mkutano wa Urusi na umoja wa mataifa ya Kiarabu mwishoni mwa juma hili utasaidia kuileta Urusi katika mstari kuhusiana na mzozo wa Syria.
Akiziita juhudi kuhusu Urusi kuwa ni zenye uzito mkubwa , Clinton amewaambia waandishi habari katika wizara ya mambo ya kigeni kuwa amezungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov mapema wiki hii, juu ya kile alichokiita, "matumaini yetu kuwa Urusi itachukua jukumu muhimu katika kumaliza mauaji na kufanyakazi kuelekea katika kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Syria.
Amesema kuwa atafuatilia siku ya jumatatu mjini New York , wakati atakapoonana na Lavrov katika majadiliano ya ngazi ya juu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa juu ya maendeleo tangu kuzuka kwa vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya Kiarabu.
zaidi ya watu 7,500 wameuwawa katika mzozo huo ambao umeanza mwaka mmoja uliopita.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae/rtre
Mhariri: Bruce Amani.