Anwaar-ul-Haq Kakar ndiye waziri mkuu wa mpito wa Pakistan
14 Agosti 2023Kakar ambaye amewakilisha jimbo la Baluchistan katika bunge la seneti tangu mwaka 2018, alikula kiapo hicho cha ofisi kilichotolewa na rais Arif Alvi ndani ya ikulu katika sherehe ya muda mfupi. Wakati wa kiapo hicho, Kakar amesema kuwa ataonesha imani ya kweli na utiifu kwa Pakistan na kwamba kama waziri mkuu wa Pakistan, atatekeleza majukumu yake kwa uaminifu, kwa uwezo wake wote, kwa mujibu wa Katiba na sheria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan . Kakar, anatarajiwa kuunda baraza la mawaziri na kuongoza serikali iliyopo hadi serikali mpya itakapochaguliwa.
Kakar ajiuzulu kutoka chama chake cha Baluchistan Awami Party
Hapo jana Kakar alijiuzulu kutoka chama chake cha Baluchistan Awami Party na kama seneta baada ya kuchaguliwa na waziri mkuu anayeondoka Shehbaz Sharif na kiongozi wa upinzani Raza Riaz kusimamia kura hiyo na kusimamia shughuli za kila siku za serikali hadi wananchi watakapochagua serikali mpya . Wakati wa kujiuzulu, Kakar alisema kuwa kutokana na jukumu muhimu alilopewa kama waziri mkuu mwenye dhamana, imemlazimu kufanya maamuzi hayo na kuomba dua kutoka kwa kila mmoja.
Serikali ya usimamizi huchaguliwa katika kipindi cha uchaguzi
Ni jambo la kawaida nchini Pakistan kuchagua serikali ya usimamizi katika kipindi cha uchaguzi. Chini ya katiba ya Pakistan, serikali ya usimamizi isiyoegemea upande wowote husimamia uchaguzi wa kitaifa ambao unapaswa kufanyika katika muda wa siku 90 baada ya kuvunjwa kwa bunge ambapo kutokana na hilo, inaamanisha kuwa uchaguzi huo unapaswa kufanyika mwezi Novemba.Hata hivyo, kura hiyo huenda ikacheleweshwa kwasababu tume ya uchaguzi inapaswa kuweka mipaka mipya kwa mamia ya maeneo bunge ya shirikisho na kimkoa na kwa kuzingatia hayo, itatoa tarehe ya uchaguzi.
Raja Riaz anaamini uchaguzi utafanyika mwezi Febrauri mwakani
Kiongozi wa upinzani anayeondoka Raja Riaz, ameliambia shirika la habari la Geo kwamba anaamini uchaguzi utafanyika mnamo Februari mwaka ujao na sio kama ilivyopangwa kabla ya mwezi Novemba. Chaguo la waziri mkuu wa serikali ya usimamizi limekuwa na umuhimu zaidi kwasababu kiongozi atakuwa na madaraka zaidi ya kufanya maamuzi ya sera kuhusu masuala ya kiuchumi.
Hafla hiyo ya kuapishwa, imefanyika wakati nchi hiyo ikisherehekea miaka 76 ya uhuru. Lakini siku hiyo imeadhimishwa huku kukiwa na machafuko ya kisiasa yanayozidi kuongezeka, ambayo yalianza baada ya kuondolewa madarakani kwa waziri mkuu wa zamani Imran Khan mwaka jana.