Argentina yaingia fainali kupitia penalti
10 Julai 2014Mlinda lango wa Argentina Sergio Romero aliokoa penalty mbili na kuipa tikiti nchi yake kushiriki katika fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1990.
Mchuano huo ulikuwa kinyume kabisa na kivumbi ambacho Ujerumani iliimiminia Brazil magoli saba kwa moja katika nusu fainali ya kwanza. Lakini Romero, ambaye hakucheza mechi nyingi katika klabu yake ya Monaco msimu uliopita, alizuia penalty zilizopigwa na Ron Vlaar na Wesley Sneijder.
Akizungumza baada ya miujiza yake, Romero alisema alikuwa na matumaini ya kuzuia penalty kadhaa na anamshukuru Mungu kuwa mambo yalimwendea sawa. Sasa anasema wameondoka uwanjani wakiwa na furaha na sasa kilichobaki ni kujiandaa sawa sawa kwa fainali. Ilikuwa ni mara ya pili kwa Uholanzi, ambao walishindwa na Uhispania katika fainali ya 2010, kuondolewa katika nusu fainali ya Kombe la Dunia kupitia matuta. Waliangushwa na Brazil mwaka wa 1998.
Arjen Robben mshambuliaji wa Uholanzi amesema walijitolea kwa moyo wote na anajivunia timu nzima. Aliongeza kuwa mchezo uliamuliwa na penalty na Wargentina wakafaulu, lakini kushindwa kwa njia hiyo inaudhi na inaumiza sana.
Matokro hayo yalikuwa mabaya sana kwa Vlaar ambaye alikuwa mwamba katika ngome ya Uholanzi katika kipindi kizimacha mchezo kwa kuwanyamazisha washambuliaji wa Argentina.
Messi hakuwa na jawabu lolote kutokana na mchezo mzuri wa beki huyo. Ijapokuwa mlinda lango Tim Krul aliokoa penalty mbili katika ushindi wa Uholanzi dhidi ya Costa Rica kwenye robo fainali, Kocha Louis van Gaal alikuwa na imani Jasper Cillessen mara hii. Lakini baadaye alikuja kujutia uamuzi huo, akisema kuwa hangeweza kufanya chochote kwa sababu alikuwa tayari amewatumia wachezaji wake watatu wa akiba.
Pia alijutia ukweli kwamba kipa wa Argentina Romero, alikuwa mwanafunzi wake wakati mmoja. Van Gaal alisema “bila shaka nilimfunza Romero namna ya kuzuia penalty kwa hivyo hilo limeniumiza”.
Romero aliokoa penalty za Vlaar na Snjeider na kuiweka Argentina katika nafasi nzuri, huku Messi, Ezequel Lavezzi na Sergio Aguero wote wakitikisa wavu. Ilikuwa zamu ya Maxi Rodriguez kupiga penalty ambayo iliwapeleka Argetina katika uwanja wa Maracana kwa fainali ya Jumapili dhidi ya Ujerumani.
Ulikuwa ni ushindi wa pili wa Argentina katika mechi tisa walizocheza na Uholanzi – na wao wa kwanza tangu fainali ya Kombe la Dunia la 1978 – na ulimwezesha Messi na wenzake kutoa heshima zao kwa gwiji wa Argentina Alfredo di Stefano, aliyeaga dunia Jumatatu mjini Madrid akiwa na umri wa miaka 88. Lakini kabla ya mpambano wa fainali, Uholanzi watashuka dimbani na Brazil siku ya Jumamosi kwa mchuano wa kumtafuta mshindi wa tatu.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman