1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armin Laschet: Kwa Urusi 'unapaswa kuzungumza zaidi'

15 Juni 2021

Mgombea ukansela wa Ujerumani kupitia muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU, Armin Laschet, amesema Ujerumani inapaswa kutafuta maeneo ya ushirikiano na Urusi, huku ikionesha upinzani kwenye masuala muhimu.

https://p.dw.com/p/3uwfx
Interview Armin Laschet | DW Global Media Forum 2021
Picha: Philipp Böll/DW

Katika mahojiano hayo aliyofanyiwa na mhariri mkuu wa DW, Manuela Kasper-Claridge, Armin Laschet, mgombea wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU, aliiambia DW Jumatatu, kwamba Ujerumani na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuacha wazi milango ya majadiliano na Moscow.

Alisisitiza kuwa licha ya tofauti na Urusi kuhusu mausala muhimu kama vile utwaaji wa kimabavu wa rasi ya Crimea, Ujerumani haipaswi kutafuta kuitenga nchi hiyo kidiplomasia.

"Watu wanaotoa miito ya msimamo mkali wanahitaji kusema nini wanachomaanisha kwa mkakati mkali," Laschet alisema. "Tuna vikwazo, lakini kukata uhusiano wa kidiplomasia au kitu kingine kama hicho itakuwa kosa."

Soma pia: Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari laanza Bonn

Mwanasiasa huyo ambaye ni waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani la North Rhine-Westphalia, alikaribisha ukweli kwamba rais wa Marekani Joe Biden atakutana na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin wiki ijayo.

"Mambo yanapokuwa magumu, unapaswa kuzungumza zaidi na siyo kwa uchache," alisema Laschet. "Ndiyo maana ni jambo zuri kwamba Joe Biden, rais wa Marekani, atakutana na rais Putin katika siku chache zizajo. Marais wa Marekani na Urusi hatimaye wanakutanan tena. Hilo ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote katika nyakati za mizozo."

DW-Intendant Peter Limbourg und NRW-Ministerpräsident Armin Laschet | DW Director General Peter Limbourg and Minister-President of the State of North Rhine-Westphalia Armin Laschet
Waziri Mkuu wa Jimbo la North-Rhine Westpahalia na mgombea ukansela wa Ujerumani Armin Laschet (kulia), akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg katika makao makuu ya DW mjini Bonn.Picha: Philipp Böll/DW

'Muungano wa mataifa ya kidemokrasia'

Laschet pia alikaribisha juhudi za Biden kushauriana na washirika wa Umoja wa Ulaya kuhusu juhudi za kukabiliana na vitendo vya uchokozi vya Urusi na China.

"Marekani inarejea kwenye Shirika la Afya Duniani, inshirikiana tena na Umoja wa Mataifa, na inahuisha mchakato wa G7, kama tulivyoshuhudia mwishoni mwa wiki," Laschet alisema. "Na naamini tunapaswa kuutumia wakati huu."

Soma pia: Warithi watarajiwa wa Merkel watofautiana kuhusu China, Urusi

"Wazo la rais la kuunda muungano wa mataifa ya kidemokrasia duniani unaofanya kazi pamoja ni fursa ya kipekaa kwa Ulaya na Ujerumani kushiriki kwa nguvu," Laschet alisema.

Kwa muktadha huu, Laschet alisema Ujerumani inapaswa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Umoja wa Ulaya.

Kuhusu Nord Stream 2

Miongoni mwa msuala yalioko msitari wa mbele katika uhusiano wa Urusi na Ujerumani ni mradi wa bomba la kusafirisha gesi la Nord Stream 2 chini ya bahari ya Baltic kwenda Ujerumani. Mradi huo unaweza kuiruhusu Moscow kuzikwepa Ukraine, Poland na mataifa mengine yanayokusanya malipo ya upitishaji kwenye ugavi wa nishati wa Urusi.

Soma pia: Mchango wa vyombo vya habari kubadili hali ya kiuchumi na kisiasa

Laschet alisema sharti la mradi huo kuendelea lilikuwa kwamba Urusi haipaswi kuruhusiwa kuutumia kuwawekea shinikizo majirani zake.

"Bomba hili halipaswi kutumiwa kuitishia Ukraine au mataifa ya Baltic au Poland,"  Laschet alisema. "Lakini, baada ya kujengwa, litakuwa sehemu nzuri ya nyongeza kwenye ugavi wa nishati."

Interview Armin Laschet | DW Global Media Forum 2021
Waziri Mkuu wa North-Rhine Westphalia Armin Laschet katika mahojiano na DW, Juni 14, 2021.Picha: Philipp Böll/DW

"Gesi itakapoanza kutoka, tunahitaji kufuatilia kanuni hizi za siasa za kijiografia kwa jicho la karibu na kuhusu ulinzi wa Ukraine," Laschet alisema. "Na hilo limekubaliwa kwa ngazi ya Ulaya pia."

Kuhusu Belarus na vikwazo

Laschet alisema vikwazo vikali vinaweza kuwa njia sahihi kuhusiana na ukandamizaji wa serikali ya taifa hilo dhidi ya upinzani tangu uchaguzi wa 2020. Ukandamizaji huu ulishuhudia hivi karibuni, kulaazimishwa kwa ndege ya abiria ya shirika la Ryan Air kutua mjini Minsk, na kumkamata mwandishi habari wa upinzani.

Mwanasiasa huyo alisema maafisa waliohusika katika ukiukaji wa haki za binadamu moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja wanapaswa kulengwa na vikwazo hivyo. Watu kama hao, alisema, walikuwa na maslahi yao ya kibiashara, akiwemo rais Alexander Lukashenko mwenyewe.

"Shughuli zao, kampuni zao, zinahitaji kuingizwa katika mfumo wa vikwazo wa Umoja wa Ulaya," Laschet alisema. "Hilo halijatokea bado. Ndiyo maana ningependa kuona: unapuzi wa vikwazo kuongeza shinikizo makhsusi kwa rais Lukashenko."

Armin Laschet ndiye mgombea wa CDU kumrithi Angela Merkel baada ya uchaguzi mkuu wa Septemba nchini Ujerumani.