1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Austria wapigakura wahafidhina wakionekana kuongoza

29 Septemba 2019

Wa Austria wanapiga kura Jumapili hii katika uchaguzi ambamo chama cha kihafidhina kinatazamiwa kushinda, lakini kitakuwa na ugumu kuunda serikali baada ya kuvunjika muungano na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/3QQnn
Österreich Wahlen Wahlkampf Wahlplakate
Picha: Reuters/L. Foeger

Chama cha Umma wa Austria ÖVP kinachoongozwa na Sebastina Kurz mwenye umri wa miaka 33, kinabashiriwa kuwa kitapata karibu asilimia 33 ya kura katika uchaguzi unaofanyika leo Jumapili.

Makadirio hayo ni juu kidogo ya kura ambazo ÖVP kilipata katika uchaguzi wa miaka miwili iliyopita lakini na hazitotosheleza kuunda serikali ya wingi wa kutosha.

Kurz "hana cha kushinda, lakini anacho cha kupoteza", kwa mujibu wa maoni ya mhariri wa gazeti la Die Presse toleo la siku ya Jumamosi. "Hata kwa ongezeko la kura Jumapili, ni vigumu zaidi kwake kuliko mwaka 2017," lilisema gazeti hilo na kuongeza kuwa hakuna mshirika anaemfaa tena.

Kukiwa na watu milioni 6.4 wenye vigezo vya kupigakura, vituo vya kupigia kura vinafunguliwa majira ya saa 7 asubuhi na kufungwa saa 11 jioni wakati ambapo makadirio ya kwanza yanatarajiwa.

Uchaguzi wa bunge ulisababishwa na sakata la rushwa la "Ibiza-gate" lililokikumba chama mshirika wa Kurz katika serikali cha mrengo mkali wa kulia FPÖ mnamo mwezi Mei, miezi 18 tu baada ya kuunda serikali ya pamoja.

Österreich Wahlen Wahlkampf Zv Debatte
Kiongozi wa chama cha ÖVP na mgombea wake mkuu Sebastian Kurz (katikati), mgombea wa chama cha Social Democratic SPÖ Pamela Rendi-Wagner (kulia) na mgombea wa chama cha FPÖ Norbert Hofer (kushoto) wakisubiri mdahalo wa TV mjini Vienna, Septemba 22,2019.Picha: Reuters/L. Foeger

Wataalamu wamebashiri kwamba huenda Kurz akashirikiana tena na chama cha Freedom (FPÖ) katika muungano mwingine uliyopigiwa debe na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na wafuasi wengine wa siasa kali za kizalendo kama ruwaza ya Ulaya nzima.

Nobert Hofer atangaza msimamo dhidi ya Strache

Lakini madai mapya ya makosa yamekitikisa chama cha hicho cha mrengo mkali wa kulia katika wiki iliyopita. Waendesha mashtaka wamethibitisha siku ya Alhamisi kwamba wanamchunguza Heinz Christian Strache, aliejiuzulu kama kiongozi wa FPÖ na naibu kansela mwezi Mei kwa sababu ya sakata la "Ibiza-gate", kuhusiana na madai ya matumizi ya udanganyifu chamani.

Kiongozi wa sasa wa chama cha FPÖ, Nobert Hofer, amesema atachukuwa hatua mara moja ikiwa makosa yatathibishwa, na kusababisha wasiwasi kwamba wafuasi wa Strache, aliekiongoza chama hicho kwa miaka 14 na anasalia kuwa na ushawishi, huenda wakajitenga na uchaguzi kupinga.

Kurz mwenyewe ameonya pia kwamba vyama vinavyoelemea mrengo wa kushoto vinaweza kupata kura nyingi zaidi ya inavyotabiriwa na kisha kuungana pamoja kuunda muungano bila yeye.

"Ikiwa kuna mabadiliko madogo tu --- basi kutakuwa na wingi dhidi yetu," Kurz aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wa mwisho mjini Vienna siku ya Jumamosi.

Österreich Wahlen Wahlkampf FPÖ Kickl
Mabango ya wagombea wa chama cha FPÖ mjini Vienna.Picha: Reuters/L. Foeger

 Tofauti na mwaka 2017, wasiwasi wa juu wa wapigakura siyo uhamiaji --- jambo la kutia moyo kwa Kurz na washirika wake wa zamani -- lakini mazingira. Mamia kwa maelf ya watu waliandamana Ijumaa mjini Vienna na miji mingine ya Austria kutaka serikali ichukuwe hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Maandamano hayo yalikuwa sehemu ya vuguvugu la maandamano ya dunia yanayoongozwa na mwanaharakati raia wa Sweden Greta Thunberg na makubwa zaidi mpaka sasa katika taifa hilo la wakaazi milioni 8.8.

Kwa mantiki hiyo, chama cha Kijani cha Austria -- ambacho kilishindwa kuingia bungeni mwaka 2017 katika matokeo ya kushtua -- kinatazamiwa kupata mafanikio makubwa safari hii. Chama hicho kinatabiriwa kuibuka na karibu asilimia 13, ongezeko la asilimia 10 kutoka matokeo ya miaka miwili iliyopita.     

Haijulikani bado, iwapo Kurz, mwanafunzi wa zamani wa sheria aliepanda haraka ngazi za madaraka katika siasa za Austria, atajaribu kuwashawishi chama kingine kidogo cha kiliberali NEOS, baada ya Jumapili kuunda nao serikali.

Kurejea kwa watetezi wa Mazingira

Kisichoshangaza kwa kuzingatia sababu za kuitisha uchaguzi wa sasa, rushwa katika masuala ya umma na ufadhili wa vyama vimekuwa mashuhuri katika kampeni, pamoja na masuala mengine ya kijamii katika vile huduma za kijamii.

Njia nyingine alio nayo Kurz inaweza kuwa kuunda serikali ya muungano na chama cha Social Democrats SPÖ. Kikitabiriwa kuwa na matokeo ya chini kabisaa ya karibu asilimia 22, chama cha SPÖ kilikuwa kinakabana koo na FPÖ kabla ya matatizo ya wiki hii kama chama cha pili kwa ukubwa nchini humo.

Österreich Wahlen Wahlkampf Grüne Werner Kogler
Mgombea mkuu wa chama cha watetezi wa Mazingira cha Austria Werner Kogler akishika bango wakati anazungumza katika mkutano wa mwisho wa kampeni mjini Vienna, Septemba 27, 2019.Picha: Reuters/L. Niesner

Tangu Vita kuu ya Pili ya Dunia, Austria imetawaliwa na aman chama cha ÖVP au SPÖ, na kwa miaka 44 jumla, vyama hivyo viwili vimeongoza pamoja, lakini Kurz ndiye alihitimisha ushirika wao wa mwisho, kuelekea uchaguzi wa 2017.

Kurz pia amezungumzia wazo la kutawala katika serikali ya wachache. Lakini hilo litanedelea mashaka ya kisiasa na kunaweza hata kusababisha uchaguzi mwingine.

Vyovyote inavyokuwa, majadiliano kati ya vyama yanatarajiwa kuchukuwa miezi kadhaa tena. Mwishowe, Rais Alexander Van der Bellen, kiongozi wa zamani wa chama cha Kijani, atahitaji kuidhinisha serikali yoyote itakayoundwa.

Serikali ya ÖVP-FPÖ ilivunjika mnamo mwezi Mei baada ya mashirika mawili ya habari ya Ujerumani kuchapisha mkanda wa vidio uliorekodiwa kwa siri katika kisiwa cha mapumziko cha Ibiza nchini Uhispania, ukimuonyesha Strache akionekana kutoa mikataba ya umma kwa kubadilishana na msaada wa kampeni kutoka muungaji bandia wa serikali ya Urusi.

Chanzo: afpe