Austria yatetea uamuzi wa kuandaa mkutano bila Ugiriki
24 Februari 2016Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Sebastin Kurz amesema viongozi kutoka mataifa tisa ya Balkan watahudhuria mkutano huo wa kilele ingawa Ugiriki haijaalikwa kwa sababu nchi hiyo haina nia ya kupunguza wimbi la wakimbizi na badala yake inataka kuendelea kuwaachia waingie kupitia Macedonia, ambako wanapata njia kuelekea ukanda wa kaskazini.
Mkutano huo uliopewa jina ''Kudhibiti Uhamiaji kwa Pamoja'' utawahusisha mawaziri wa mambo ya nje na wale wa mambo ya ndani kutoka Albania, Bosnia, Bulgaria, Croatia, Kosovo, Macedonia, Montenegro, Serbia na Slovenia. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Karl-Heinz Grundboeck amesema mikutano kama hiyo huwa inafanyika kwa kuzingania mfumo na washiriki wa kudumu.
Mawaziri hao watajadiliana masuala kadhaa kama vile uangalizi na udhibiti wa mikapa na jinsi ya kukabiliana na magenge yanayofanya biashara ya kuwasafirisha binadamu kimagendo, pamoja na kuimarisha utoaji wa taarifa kuhusu sera za nchi zao. Mkutano huo wa Vienna pia utajaribu kuwa na msimamo wa pamoja kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika siku ya Alhamisi.
Austria yaikasirisha Ugiriki
Hata hivyo, uamuzi huo wa Austria umeikasirisha Ugiriki ambayo imetoa lalamiko la kidiplomasia dhidi ya mkutano huo iliyouita usio wa kirafiki. Wizara ya mambo ya nje ya Ugiriki imesema kutengwa kwake kunamaanisha mkutano huo wa kilele ni jaribio la kuchukua maamuzi bila ya nchi hiyo kuwepo, ambayo moja kwa moja inaiathiri nchi hiyo pamoja na mipaka yake.
Ugiriki imeilalamikia hatua ya Austria, ikisema kuwa mkutano huo ni sawa na usiokuwa wa kirafiki na unaopingana na sera za Ulaya.Sera ya hivi karibuni ya Macedonia ya kukataa kuingia kwa raia wa Afghanistan, ambao ni moja ya makundi makubwa ya wahamiaji, tayari imesababisha mrundikano mkubwa kwenye mpaka wa Ugiriki. Maafisa wa Ugiriki wameukosoa mkutano huo wakisema unadhoofisha juhudi za kuwa na uamuzi wa pamoja wa Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia suala la mzozo wa wakimbizi.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras amemwambia waziri mkuu mwenzake wa Uholanzi, Mark Rutte, kwamba maamuzi kuhusu wimbi la wakimbizi lazima liangaliwe kwa pamoja bila ya nchi yoyote kutengwa. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya pia imekosoa hatua za hivi karibuni za kuwazuia wakimizi katika njia ya Balkan, ikisema kuwa ni kinyume cha sheria.
Ama kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Sebastin Kurz, ameikosoa sera ya Ujerumani kuhusu wakimbizi, akisema inakanganya. Amesema mwaka uliopita, Austria ilikubali mara mbili zaidi ya maombi ya watu wanaoomba hifadhi kama ilivyokuwa kwa Ujerumani na kusisitiza kuwa hilo halitotokea kwa mara ya pili.
Kurz pia amezungumzia ukosoaji uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere kuhusu sera ya Austria ya kuweka kiwango maalum cha wakimbizi 80 wanaoomba hifadhi kuingia nchini humo kwa siki, huku ikiwaachia wengine 3,200 kwenda nchi nyingine, ingawa wengi wao huelekea Ujerumani.
Waziri huyo amesisitiza kuwa Austria inataka kushirikiana na Ujerumani, hivyo wanatarajia kwamba Ujerumani itasema kama imeajiandaa au haijajiandaa kuwapoka wakimbizi, au kama haiko tena tayari kuwapokea. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria, Johanna Mikl-Leitner amesema ana matumaini kwamba watapata jibu pa pamoja na Umoja wa Ulaya na kwamba inabidi kwa sasa wapunguze wimbi la wakimbizi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE, AFPE, DPAE, RTRE,http://bit.ly/1mXkpoK
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman