1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa

Admin.WagnerD22 Oktoba 2015

Zaidi ya watu 30,000 katika maeneo ya vita nchini Sudan Kusini wanaweza kufa njaa. Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Alhamisi (22.10.2015) imeonya wengine maelfu kwa maelfu wako kwenye hatari ya kupoteza maisha,

https://p.dw.com/p/1GsnT
Watoto wanaokabiliwa na utapia mlo Sudan Kusini.
Watoto wanaokabiliwa na utapia mlo Sudan Kusini.Picha: Getty Images/AFP/N. Sobecki

Wakati tangazo rasmi la njaa halikutolewa repoti hiyo inaelezea jinsi hali ilivyo mbaya sana kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 22 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoandamana na ukatili na tuhuma za uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kwa huduma za ugawaji wa chakula.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) pamoja na shirika la Mpango wa Chakula la umoja huo (WFP) yamesema katika taarifa ya pamoja kwamba takriban watu 30,000 wanaishi katika hali mbaya sana na wanakabiliwa na njaa na kifo.

Jimbo lililoathiriwa zaidi ni la Unity lenye mapigano kaskazini mwa nchi hiyo jimbo ambalo lilikuwa ndio lenye kuzalisha mafuta kwa wingi nchini humo lakini hivi sasa ndiko yalikochaga mapigano na eneo lenye utekaji nyara mkubwa na ubakaji wa watoto na wanawake.

Baa la njaa

Takriban watu milioni 3.9 wako katika hali hiyo ya maafa ambapo ni theluthi moja ya idadi ya watu nchini humo ongezeko la asilimia 80 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.

Wanajeshi wa Sudan Kusini.
Wanajeshi wa Sudan Kusini.Picha: picture-alliance/dpa/M. Knowles-Coursin

Repoti ya Shirika lenye Kuratibu na Kuorodhesha Usalama wa Chakula imeonya Alhamisi bila ya kuchukuliwa kwa hatua za dharura na za haraka kutowa msaada wa kibinaadamu hali hiyo itazidi kuwa mbaya kufikia kiwango cha baa la njaa.

Wakati uhaba wa mvua umeathiri mavuno katika baadhi ya maeneo hali mbaya zaidi inakutikana katika maeneo ya vita ambayo imechangiwa zaidi na mizozo na sio hali ya hewa.

Kaunti zllizoathirika vibaya ni za Leer,Guit,Koch na Mayendit ambapo mashirika ya misaada yamelazimika kuondoka katika miezi ya hivi karibuni kutokana na mapigano kuwa makali.

Maafa yanaweza kuepukwa

Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula kwa Sudan Kusini Joyce Luma amesema watu wako kwenye ukingo wa maafa ambayo yanaweza kuepukwa.

Wakimbizi wa Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan Kusini.Picha: Getty Images/AFP/Z. Abubeker

Pande zote mbili katika mzozo huo wa Sudan Kusini zinatuhumiwa kwa kufanya mauaji kwa misingi ya kikabila, kuwasajili watoto jeshini na kuwauwa pamoja na kufanya ubakaji kila mahala,kuwatesa wananchi na kuwapotezea makaazi yao kwa kutumia nguvu kwa lengo la kuwatokomeza maadui zao kwenye maeneo wanayoyadhibiti.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) kwa Sudan Kusini Jonathan Veitch anasema tokea mapigano yazuke karibu miaka miwili iliopita watoto wamekuwa wakiathirika na mzozo, magonjwa,hofu na njaa.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/dpa

Mhariri :Hamidou Oummilkheir