Baba wa mshambuliaji wa bomu Manchester akamatwa
25 Mei 2017Wakati maombolezo yaliyochanganyika na hasira kuhusiana na kuvuja kwa taarifa nchini Marekani zinazohusiana na uchunguzi wa tukio hilo yakiendelea, taarifa zinasema baba yake mshambuliaji Salman Abedi alikuwa mmoja wa wanamgambo wa kundi la itikadi kali lenye mafungamano na al-Qaeda.
Nchi ya Uingereza ambayo ilikumbwa na mshituko baada ya shambulio hilo la kigaidi , ilitulia kwa muda wa dakika moja kuanzia saa tano asubuhi saa za Uingereza kuwakumbuka watu 22 waliofariki katika shambulio hilo, wahanga ambao hawana hatia katika shambulio la hivi karibuni kabisa lililodaiwa na kundi la Dola la Kiislamu kwamba wao ndio walifanya shambulizi hilo.
Na wakati majina zaidi ya watoto yakitajwa miongoni mwa wahanga wa mauaji ya siku ya Jumatatu, maafisa nchini Libya walimkamata baba wa mshambuliaji huyo pamoja na kaka yake wakati polisi nchini Uingereza walifanya msako mwingine na kuwakamata watu wengine.
Watu zaidi wakamatwa
Baba yake Abedi, Ramadan , "alikuwa mmoja wa wanamgambo wa kundi la Libyan Islamic Fighting Group LIFG," amesema Ahmed bin Salem , msemaji wa majeshi ya Libya, ambayo yanachukua nafasi ya polisi katika serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya.
Ramadan Abedi alikuwa akisakwa na utawala wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi kwa mahusiano yake na kundi lililopata ukimbizi Uingereza kabla ya kurejea nchini Libya mwaka 2011 na kujiunga na vuguvugu la mapinduzi yaliyokuwa yakiungwa na NATO ambayo hatimaye yaliuondoa utawala wa Gaddafi.
Kundi hilo ambalo hivi sasa limevunjwa lilianzishwa mwaka 1995 na Walibya ambao walipigana na majeshi ya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti nchini Afghanistan na kuendelea kubakia huko baada ya majeshi hayo kujiondoa.
Lengo pekee la kundi hilo lilikuwa kuuondoa utawala wa Gaddafi.
Mshambuliaji huyo wa kujitoa muhanga Salman Abedi huenda alitengeneza mwenyewe bomu alililoliripua ama alipata msaada fulani kutoka kwa mshirika wake, duru zenye vyanzo karibu na uchunguzi zimeliambia shirika la habari la Reuters. Polisi wamesema leo wamewakamata watu muhimu na kugundua vitu muhimu wakati wakichunguza shambulio hilo la bomu mjini Manchester.
Polisi ya Manchester inawashikilia kwa sasa watu wanane, baada ya kumwachia huru mwanamke leo bila ya kumfungulia mashitaka. Taarifa zinasema pia kwamba mshambuliaji huyo alisimama kwa muda katika uwanja wa ndege wa Istanbul kabla ya kwenda kufanya shambulio hilo.
Serikali ya Marekani kuchukua hatua
Wakati huo huo mwanadiplomasia mwandamizi zaidi wa Marekani nchini Uingereza Lewis Lukens , ameshutumu uvujishaji wa taarifa kwa vyombo vya habari, akisema serikali ya Marekani itachukua hatua kuwataja wale waliohusika. Mchambuzi wa masuala ya usalama na afisa wa zamani wa ujasusi Bob Ayers amesema hali hiyo itafikia mwisho hivi karibuni.
"Mara ya mwisho nilipoangalia polisi ya manchester haikuzungumza kwa niaba ya Uingereza, haizungumzi kwa mikataba ya kimataifa, kwa hiyo polisi ya Manchester huenda ikakasirishwa lakini yatakwisha."
Na nchini Uingereza polisi wenye silaha wanafanya doria katika treni nchini humo kuanzia leo kwa mara ya kwanza , polisi inaohusika na masuala ya usafiri imesema , baada ya kiwango cha hofu ya ugaidi kupandishwa kuwa hali mbaya kufuatia shambulio mjini Manchester.
Navyo vilabu viwili maarufu mjini Manchester , United na City vimechangia kiasi ya pauni milioni moja katika mfuko wa dharura ulioundwa baada ya shambulio katika mji huo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf , Saumu