1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado kuna maswali muhimu yanahitaji majibu kuhusu Mpox

22 Agosti 2024

Wakati hofu ya kusambaa kwa maradhi ya homa ya nyani duniani ikizidi, bado kuna maswali mepesi kama vile hatari ya ugonjwa huo na tafauti baina ya aina za virusi vyake hadi sasa hayako wazi wala hayana majibu mepesi.

https://p.dw.com/p/4jnmH
Mtaalamu kutoka kampuni ya Denmark ya kutengeneza dawa ya Bavarian Nordic
Mtaalamu kutoka kampuni ya Denmark ya kutengeneza dawa ya Bavarian NordicPicha: Bavarian Nordic/abaca/picture alliance

Mnamo mwezi Julai, Shirika la Afya Duniani, WHO, lilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa maradhi ya homa ya nyani, ambayo kwa mara ya kwanza yaligundulika miongoni mwa wanaadamu mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa miongo kadhaa sasa, ugonjwa huo ulikuwa umejikita kwenye mataifa machache tu ya Afrika, huku idadi ya vifo ikiwa ni asilimia moja hadi kumi miongoni mwa wale wanaoambukizwa.

Hali ya wasiwasi ilianza kuwa kubwa kutoka mwaka 2022, pale ugonjwa huo ulipoanza kusambaa kwengineko ulimwenguni, hasa mataifa ya Kimagharibi, ingawa idadi ya wanaopoteza maisha kwenye mataifa mapya maradhi hayo yalikoingia ni cha chini sana, kiasi ya asilimia 0.2 tu. Tafauti hii inatokana na aina tafauti za virusi vya homa ya nyani na pia kutokana na mifumo ya kiafya.

Mathalani, mtu anayeishi Marekani ama Ulaya ana nafasi nzuri zaidi ya kupata huduma zinazofaa na kwa wepesi kuliko aliyeko mataifa ya Afrika.

Mtaalamu wa virusi, Antoine Gessain, anasema hatari ya homa ya nyani inategemea sana na kiwango cha huduma za msingi za kiafya. Kiwango cha sasa cha maambukizo, ambacho ni asilimia 3.6, kingelikuwa cha chini zaidi endapo yangelikuwa nje ya Kongo.

Soma pia:Tanzania yaimarisha hatua za kuzuia maambukizi ya Mpox

Sababu nyengine ya inayoongeza idadi ya vifo ni pamoja na kwamba baadhi ya wagonjwa wako rahisi zaidi kupata maambukizo mengine kuliko wenzao.

Katika vifo 500 miongoni mwa watu 15,000 walioambukizwa, wengi wao ni watoto waliokwishateseka vibaya kwa ukosefu wa lishe.

Inapolinganishwa na mwaka 2022-23, ambapo idadi ya waliokufa ilikuwa ndogo - kiasi 100 katika wagonjwa 100,000 - wengi wao wakiwa wanaume ambao tayari afya zao zilishakuwa mashakani kutokana na kuwa tayari waathirika wa virusi vya Ukimwi.

Tafauti ya idadi ya vifo pia inaweza kuelezeka kwa jinsi maambukizo yenyewe yalivyopatikana. Katika mwaka 2022-2023, maambukizo mengi yalitokea kupitia matendo ya ngono.

Mkanganyiko wa aina ya kirusi kinachoambukiza

Sababu nyengine inayoongeza mkanganyiko ni aina ya kirusi, au familia ya kirusi kilichosababisha maambukizo.

Maambukizo ya mara mwaka 2022-2023 yalisababishwa na aina ya kirusi cha homa ya nyani kiitwacho Clade 2, ambacho zaidi kiko magharibi mwa Afrika ingawa pia kiligundulika Afrika Kusini.

Chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Nyani imepatikana

Maambukizo ya Kongo yanatokana na aina ya kirusi kiitwacho Clade 1, kinachopatikana zaidi kwenye maeneo ya kati ya nchi hiyo.

Lakini maambukizo ya mara ya pili yanayowaathiri wanaume watu wazima nchini humo yanahusishwa zaidi na kirusi aina ya 1b.

Mkanganyiko huu umevifanya vyombo vya habari kueleza kuwa kirusi aina ya 1b ni hatari zaidi kuliko aina za virusi vya homa ya nyani vilivyowahi kutokea huko kabla.   

Soma pia:Uingereza yaiahidi Kongo pauni milioni 3.1 katika jitihada za kudhibiti mpox

Mtaalamu wa virusi nchini Uholanzi, Marion Koopmans, anasema kwamba madai haya ya vyombo vya habari ni makubwa zaidi kuliko ushahidi uliopo kwenye makali na kasi ya maambukizo ya aina mpya ya kirusi cha 1b.

Mtaalamu huyo anasema kinachofahamika kwa uhakika ni kwamba aina ya kirusi ya Clade 1 inahusiana na maradhi mabaya zaidi kuliko Clade 2.

Hata hivyo, watafiti wanatoa wito wa tahadhari kuchukuliwa kabla ya kutoa hitimisho. Tayari aina hiyo ya kirusi imegundulika nchini Sweden.