1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado kuna taharuki New-Delhi

25 Desemba 2012

Msemaji wa polisi amefahamisha kwamba sehemu kubwa ya katikati ya mji huo imeendelea kufungwa kufuatia ghasia zilizozusha wasiwasi na Taharuki nchini India.

https://p.dw.com/p/178u0
Maandamano dhidi ya ukatili wa wanawake India
Maandamano dhidi ya ukatili wa wanawake IndiaPicha: Reuters

Polisi aliyejeruhiwa katika ghasia wakati wa maandamano ya kupinga kitendo cha ubakaji wa mwanafunzi mmoja wa kike, mjini New Delhi amefariki hii leo (25.12.2012).

Polisi Konstable huyo, Subash Tomar aliyekuwa na umri wa miaka 47 alipelekwa katika eneo la lango la sanamu la India siku ya Jumapili kudhibiti ghasia za waandamanaji ambako alipigwa na kundi la waandamanaji hao kabla ya kupelekwa hospitali na polisi wenziwe.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi ya New Delhi Rajan Bhagat, hadi sasa watu 8 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kushtakiwa kwa mauwaji. Msemaji huo wa polisi amefahamisha kwamba watu hao wametumia fimbo na kumshambulia kwa kumpiga mawe polisi huyo.

Indien Vergewaltigung Proteste
Picha: Raveendran/AFP/Getty Images

Tomar amezikwa leo Jumanne (25.12.2012) baada ya mwili wake kuchomwa huko New Delhi kama ilivyo desturi ya Wahindu na kupewa heshima za mwisho za kiserikali. Itakumbukwa kwamba zaidi ya polisi 50 walijeruhiwa katika ghasia za Jumapili wakati walipokuwa wakijaribu kuyazima maandamano yaliyoenea ya kupinga uhalifu wa ubakaji unaoshuhudiwa nchini India.

Maandamano hayo yalichochewa na tukio la kubakwa na genge la watu mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 23 mnamo Desemba 16 pamoja na kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake nchini humo.

Hali ya kiafya ya msichana huyo inasemekana imekuwa mbaya kufikia Jumatatu usiku na bado anaendelea kutibiwa akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi huku akiwa bado anakabiliwa na matatizo ya kupumua.

Waziri mkuu wa India ManMohan Sighn akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni siku ya Jumatatu ametoa mwito wa kuwepo utulivu kufuatia ghasia hizo na kuahidi kwamba waliohusika katika kitendo hicho cha ubakaji wataadhibiwa kwa uhalifu huo. Aidha rais wa nchi hiyo Pranab Mukherjee amewaasa vijana kudumisha sheria na utulivu badala ya kuchukua hatua za kulipiza kisasi kwa kuingia mitaani na kufanya fujo.

Katika siku ya sikukuu ya Krismasi inayosherehekewa na Wakristo duniani kote polisi imezifunga barabara zote za kuelekea lango kuu la kuingia mjini New Delhi ambako kumegeuka kuwa kituo cha maandamano ambayo yanafanywa zaidi na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Waandamanaji waliojitokeza kote nchini India katika kipindi cha zaidi ya wiki moja kupinga kitendo cha ubakaji wameilaani idara ya polisi na serikali kwa kuzembea katika kukabiliana na uhalifu huo. Maandamano makubwa zaidi yameshuhudiwa mjini New Delhi siku ya Jumapili hali iliyowafanya polisi kuyafunga maeneo yote ya kuelekea katika majengo ya ofisi za serikali.

Waziri mkuu wa India Manmohan Singh
Waziri mkuu wa India Manmohan SinghPicha: picture-alliance/Bildfunk

India, nchi ya kihafidhina ambayo uchumi wake unakuwa kwa haraka imetowa nafasi kubwa ya ajira kwa wanawake na kuwafanya kujitegemea zaidi kifedha, lakini wanaharakati wanasema hali hiyo haiwafurahishi wanaume ambao wanahisi mtindo huo ni kitisho kwa mfumo dume wa taifa hilo. Takribani asilimia 90 ya visa 256,329 vya kikatili vilivyonakiliwa mwaka jana vilikuwa ni dhidi ya wanawake huku idadi ya waliobakwa katika mji mkuu wa nchi hiyo ikiongezeka kwa asilimia17 mwaka huu.

Mwandishi: Saumu Yusuf

Mhariri: Bruce Amani