Bajeti ya Malawi bado imekwama.
1 Septemba 2007Matumizi ya serikali yaliweza tu kutolewa hapo mwezi wa Julai baada ya bunge kumruhusu waziri wa fedha kutumia hadi dola milioni nane hatua ambayo imechukuliwa baada ya serikali kuomba dola milioni 32 kugharamia shughuli za utumishi serikalini kwa miezi minne.
Tayari kuna uwezekano wa kuzuka uhaba wa madawa katika hospitali kubwa kabisa ya rufaa nchini humo Hospitali ya Queen Elizabeth na kwengineko.
Mkuu wa hospitali hiyo Thom Chisale amekaririwa akisema kwamba kwa kawaida kituo hicho cha matibabu hupata fedha za serikali katika wiki ya kwanza ya kila mwezi lakini iwapo bajeti hiyo haitopitishwa hivi karibuni taathira yake itakuwa uhaba mkubwa wa madawa nchi nzima.
Wafanyakazi katika sekta ya utumishi serikalini ambayo ndio yenye kuwajiri watu wengi kabisa takriban 120,000 wakiwemo kwenye orodha ya kulipwa mishahara wana wasi wasi wapi itatoka hundi ya mshahara wa mwezi wa Augusti iwapo mgogoro huo wa bajeti utaendelea na huenda wafanyakazi hao wakaishtaki serikali iwapo hawatolipwa mshahara wao wa Augusti kwa wakati.
Kuidhinishwa kwa bajeti hiyo ya dola bilioni 2.1 awali kulicheleweshwa kutokana na kifo cha Mke wa Rais Ethel Mutharika aliefariki hapo mwezi wa Mei.
Baadae taratibu za kuidhinisha bajeti hiyo zikakwama kutokana na malumbano ya kisiasa yaliochochewa na hukumu ya Mahkama Kuu iliotolewa tarehe 15 mwezi wa Juni yenye kumruhusu spika wa bunge kuwatimuwa wabunge walioasi vyama vyao ambavyo walitumia tiketi zake wakati walipochaguliwa kwenye bunge la taifa hapo mwaka 2004.
Rais Bingu wa Mutharika mwenyewe binafsi alikitelekeza chama UDF baada ya kukosana na Rais aliemtangulia Bakili Muluzi na baadae aliunda kundi lake mwenyewe la kisiasa la DPP ikiwa ni miezi tisa tu baada ya kuchaguliwa.
Wakati urais wa Mutharika hautoathirika na hukumu hiyo takriban wabunge 60 waliojiunga na chama chake cha DPP wako katika hatari ya kupoteza viti vyao.Uamuzi huo wa mahkama unaweza kukibakishia chama chake viti vitano tu bungeni.
Hata hivyo mmojawapo ya wabunge waathirika wa hukumu hiyo Yunus Mussa baadae aliwasilisha pingamizi ya kisheria iliomzuwiya spika kutekeleza hukumu hiyo ya Mahkama Kuu. Wabunge wa upinzani ambao hivi sasa ndio walio wengine bungeni wamegoma kujadili bajeti hiyo ya taifa hadi hapo pingamizi hiyo ya kisheria iliowasilishwa na Mussa itakapondolewa.
Serikali ya Uingereza ambayo ndio mfadhili mkuu wa nchi hiyo tayari imeyataka makundi hayo hasimu kuondowa tafauti zao. Uingereza inaipatia nchi hiyo ya kusini mwa Afrika dola milioni 141 kila mwaka.
Kuna uwezekano pia kwa sarafu ya nchi hiyo kwacha kushuka thamani kwenye masoko ya kimataifa jambo ambalo litapandisha bei za bidhaa muhimu kama vile chakula,mafuta na mbolea na hiyo kuwa pigo kwa wananchi wengi wanaopambana na umaskini nchini humo.
Wakati haijulikani lini bajeti hiyo inaweza kupitishwa kumekuwepo na maadamano kila siku nchini kote Malawi na wananchi wamekuwa wakipiga honi za magari,kengele za baiskeli na filimbi kila siku saa moja na nusu asubuhi,saa sita na nusu mchana na saa 11 na nusu jioni kupinga kushindwa kwa bunge kupitisha bajeti hiyo ya taifa.