Baraza la Habari Kenya na hofu ya upotoshaji wa matokeo
11 Agosti 2022Ucheleweshwaji wa matokeo rasmi kutoka kwa Tume ya Uchaguzi nchini humo, IEBC umesababisha kuenezwa kwa taarifa nyingi potofu na baraza hilo sasa linaangazia tatizo hilo.
Baraza hilo linalowasimamia waandishi wa habari, limeeleza kwamba linafanya mashauriano na muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na wahariri ili kuweza kubuni njia ya pamoja ya kupeperusha matokeo kati ya vyombo vya habari nchini.
Matokeo tofauti
Kupitia taarifa kwa waandishi wa habari, baraza hilo limeelezea wasiwasi kwamba baadhi ya vituo vya habari vinatangaza matokeo ambayo ni tofauti kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika wiki hii, ilhali wote wanayatoa matokeo hayo kutoka kwenye tovuti ya tume ya kitaifa ya uchaguzi, IEBC.
Taswira inayojitokeza ni kwamba yule mgombea urais anayeongoza inategemea chombo cha habari unachokitazama. Afisa Mkuu Mtedaji wa MCK David Omwoyo anasema kwamba hatua hiyo inachangia kuibua taharuki kati ya umma wakati huu ambapo subira ya muda mrefu ya matokeo ya uchaguzi inawatatiza wengi.
Kufikia sasa tume ya IEBC imetangaza kwamba imepokea asilimia 99 ya fomu za 34A zinazosheheni matokeo ya uchaguzi wa urais yanayowakilisha vituo vya kupiga kura 45,653 kati ya 46,229.
Zoezi la ujumlishaji wa matokeo bado linaendelea kwenye maeneo mengine nchini na kama alivyoeleza mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, akisema sheria ya Kenya inawapa hadi siku saba kukamilisha shughuli ya kuhesabu kura na kumtangaza mshindi.
Uchelewaji wa matokeo wachangia
Ucheleweshwaji wa matokeo ya uchaguzi umechangia sana uenezaji wa taarifa potofu katika vyombo vya habari na pia kwenye mitandao ya kijamii. Wananchi wanaonekana kufuata zile taarifa zinazowavutia ama yale wanayoazimia kuwa ukweli kulingana na kiongozi wanayemuunga mkono.
Kadhalika, Afisa Mkuu Mtedaji wa baraza la vyombo vya habari nchini Kenya, David Omwoyo amesisitiza kuhusu maslahi na usalama wa waandishi habari kipindi wanapofuatilia matokeo ya uchaguzi mkuu.
Aidha, Wakenya wanakanganyika na namna baadhi ya wagombea wa viti mbalimbali vya kisiasa wameanza kutoa ujumbe wa shukrani wakiashiria kupata ushindi kwenye uchaguzi huu mkuu, na kutoa ahadi za uongozi mwema, ilihali kwenye maeneo hayo bado matokeo rasmi hayajatangazwa.