Baraza la Usalama laahirisha kura juu ya vita ukanda wa Gaza
20 Desemba 2023Wanadiplomasia kadhaa wameliambia shirika la habari la dpa kwamba kura hiyo sasa imepangwa kufanyika baadaye leo.
Rasimu ya azimio lililowasilishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu limehimiza kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza ili kutoa fursa ya kupelekwa misaada zaidi ya kibinadamu.
Marekani, mshirika wa karibu wa Israel na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na yenye nguvu ya kura ya turufu, imepinga matumizi ya neno "kusitisha mapigano" kwenye azimio hilo.
Mwanadiplomasia mmoja kutoka nchi mwanachama wa Baraza la Usalama ameeleza kuwa kusogezwa mbele kwa kura hiyo kumefanyika ili kuishawishi Marekani kutotumia kura ya turufu kupinga rasimu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linahimiza kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza.