1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lailaani Syria

Admin.WagnerD5 Oktoba 2012

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi yaliyofanywa na Syria siku ya Jumatano katika mpaka wa Uturuki ambayo yameuwa watu watano.

https://p.dw.com/p/16L0y
Picha: AP

Baraza hilo limesema kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa sheria za kimataifa na ni lazima kikome kisirudiwe tena siku zijazo. Tamko la Baraza hilo lenye wanachama 15 limesema kuwa mashambulizi za kimataifa na ni lazima kikome mara moja na kisirudiwe tena siku zijazo. hayo yameonyesha ni kwa kiasi gani mzozo unaoendelea nchini Syria una athari za kiusalama kwa mataifa ya jirani na eneo la mashariki ya kati kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametaka kuwepo kwa utulivu wakati huu ambapo bunge la Uturuki tayari limeshapitisha uamuzi wa kuichukulia hatua za kijeshi Syria katika kipindi cha mwaka unaokuja kuwalinda raia wake mpakani.

Ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa ugomvi baina ya mataifa hayo na kusema kuwa hatari ya kuzuka kwa mzozo mkubwa katika eneo la mashariki ya kati inazidi kuongezeka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: Getty Images

Urusi na pingamizi lake

Tamko la baraza la usalama linatolewa baada ya Urusi kukataa tamko lililoandaliwa mara ya kwanza linaloilaani Syria na badala yake ikaja na tamko lake ambalo limefanyiwa mabadiliko linalozitaka zote Syria na Uturuki kujizuia na mashambulizi.

Mataifa ya magharibi yalikataa andiko hilo la Urusi hivyo likaamua kutumia andiko la kwanza lakini likaongeza vipengele baadhi kutoka katika lile la Urusi.

Vladimir Putin, Rais wa Urusi
Vladimir Putin, Rais wa UrusiPicha: AFP/Getty Images

Kwa upande wa Syria Balozi wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa Bashar Jafaar ameomba radhi na kusema kuwa hawakuwa wanatafuta kuzusha ugomvi na Uturuki wala nchi nyingine yoyote, na kwamba serikali ya Syria ingelilifanyia uchunguzi tukio hilo.

"Mamlaka zenye uwezo kamili za Syria zinathibitisha kwamba zinachunguza kwa umakini mkubwa chanzo cha moto uliosababisha vifo vya raia wa Uturuki."alisema Jaffar.

Balozi Jaffari ameongeza kuwa serikali ya Syria ina nia hasa ya kulinda ujirani mwema na Uturuki. Kama ikitokea tukio lolote kwenye baina ya nchi mbili, basi serikali za nchi husika zinatakiwa kutumia busara, mantiki na kuzingatia sababu za tukio hilo.

Aidha, ametoa wito kwa Uturuki kushirikiana na Syria kuyadhibiti makundi yaenye silaha kuingia kupitia mpaka baina yao na kufanya mashambulizi nchini mwake.

Kisasi cha Uturuki

Tangu kutokea kwa tukio hilo Uturuki imekuwa ikifanya mashambulizi katika maeneo muhimu ya Syria yaliyoko mpakani kwa siku ya pili mfululizo. Waziri Mkuu wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan amesema kuwa nchi yake kamwe haina lengo la kuanzisha vita na kwamba uamuzi wa bunge wa kuanzisha operesheni za kijeshi mpakani ni kwa ajili ya kujilinda.

Recep Tayyip Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki
Recep Tayyip Erdogan Waziri Mkuu wa UturukiPicha: picture alliance/dpa

Licha ya kauli hiyo ya Erdogan raia wa Uturuki katika eneo hilo la mpaka wamekumbwa na hofu kubwa. Wakizungumza na shirika la habari la Reuters hii leo wengi wameelezea wasiwasi wao kuwa hatua hiyo huenda ikaichochea Syria kufanya mashambulizi zaidi.

Nayo Marekani imezungumzia mashambulizi hayo ikisema kuwa Uturuki imechukua hatua sahihi na inayofaa kujibu kitendo cha Syria. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani, Victoria Nuland, amesema na hapa ninamnukuu" kwa mtazamo wetu, hatua iliyochukuliwa na Uturuki ni sawia kabisa." mwisho wa kumnukuu.

Mwandishi: Stumai George/Reuters /AFP

Mhariri: Josephat Charo