1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Baraza la Usalama limewatelekeza Wasyria"

Mohammed Khelef12 Machi 2015

Zaidi ya mashirika 20 ya misaada yamelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuwalinda Wasyria katika wakati ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vinatimiza mwaka wa nne.

https://p.dw.com/p/1Ep4V
Sehemu ya eneo la Jobar karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kushambuliwa na ndege za jeshi.
Sehemu ya eneo la Jobar karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kushambuliwa na ndege za jeshi.Picha: REUTERS/B. Khabieh

Mashirika hayo, yakiwemo Kamati ya Kimataifa ya Uokozi, Baraza la Wakimbizi la Norway na Handicap International, linalojihusisha na watu wenye ulemavu duniani, yamesema Baraza la Usalama limeshindwa kutekeleza mapendekezo matatu yaliyopitishwa na chombo hicho mwaka jana, yaliyokusudiwa kuimarisha misaada ya kibinaadamu kwa raia wa Syria.

Miongoni mwa maazimio hayo ni Azimio Namba 2139 la mwaka 2014, ambalo linasomeka kuwa limepitishwa ili kuwajengea matumaini watu wa Syria, lakini badala yake mwaka huo pekee watu 76,000 wakauawa.

Kwa mujibu wa ripoti yao iliyochapishwa leo, mzozo na maafa ya kibinaadamu nchini Syria vimepanda juu, hali msaada wa kiutu na fursa ya kuwafikia wenye shida ikishuka katika kiwango kinachoogofya, huku wafadhili wa kimataifa wakitelekeza jukumu lao.

"Eneo hili hivi sasa lina idadi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani, takribani asimilia 53 ya wakimbizi duniani wanakutikana kwenye eneo la Arabuni, ambao nao wengi wao ni kutoka Syria. Idadi ya wakimbizi waliokimbia nchi hiyo ni takribani milioni tatu na wale waliogeuzwa wakimbizi wa ndani ni milioni saba na nusu. Idadi hii ni kubwa sana, ambayo ina athari za muda mrefu si kwa Syria pekee, bali kwa eneo zima," anasema Maya Yahya wa Carnagie Middle East Center, taasisi ya inayojihusisha na utafiti wa sera za kijamii katika eneo la Mashariki ya Kati.

Hakuna matumaini

Ripoti hii imetolewa katika wakati ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vikitimiza mwaka wa nne na kukiwa hakuna ishara ya kumalizika. Hadi sasa vita hivyo vimeshaangamiza maisha ya watu 200,000 na kuwageuza nusu ya raia milioni 23 wa nchi hiyo kuwa wakimbizi.

Ukurasa maalum wa Facebook kwa ajili ya miaka minne ya vita vya Syria ukiuliza "watu wangapi tena wafe ili itoshe kwa jamii ya kimataifa kuikoa Syria."
Ukurasa maalum wa Facebook kwa ajili ya miaka minne ya vita vya Syria ukiuliza "watu wangapi tena wafe ili itoshe kwa jamii ya kimataifa kuikoa Syria."Picha: Facebook

Robert Lindner wa shirika la misaada la Oxfam nchini Ujerumani ameiambia Deutsche Welle kwamba watu wengi zaidi nchini Syria wanazidi kujikuta wakikwama mbele ya mstari wa mapigano na hawana namna yoyote ya kupata msaada wa kibinaadamu, huku wale wanaopata nafasi ya kukimbia nchi hiyo, wakiachwa kuteseka na kupoteza maisha katika mataifa jirani wanayokimbilia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya Wasyria walioko kwenye maeneo ambayo hawawezi kufikiwa imepanda kutoka milioni mbili unusu mwaka 2013 hadi milioni tano mwaka huu, miongoni mwa sababu zikiwa ni serikali ya Syria kuyazuia mashirika ya misaada.

Miaka minne baada ya upinzani wa kisiasa kugeuka uasi wa silaha, hali nchini Syria imeruhusu siasa za kimataifa na kikanda kuingilia hatima ya raia wa kawaida, ambapo ripoti hiyo inasema sasa mzozo huo umekuwa vita vya kisiasa vinavyoshirikisha pande nne - serikali ya Syria, makundi ya Kiislamu, wapinzani wa serikali na mataifa ya kigeni.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou