1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama: Mchakato wa kisiasa Syria uwe jumuishi

18 Desemba 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuanzishwa mchakato wa kisiasa nchini Syria utakaokuwa "jumuishi na kuongozwa na Wasyria wenyewe" baada ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/4oHSh
Ukumbi wa mikutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York
Ukumbi wa mikutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Kwenye tamko lake kwa vyombo vya habari lililotolewa usiku wa kuamkia leo, Baraza hilo limesema watu wa Syria inafaa wapatiwe nafasi ya kuamua hatma ya taifa lao na kulisuka upya kisiasa kwa njia ya amani, uhuru na kidemokrasia.

Chombo hicho chenye dhima ya kusimamia usalama na amani duniani pia kumewarai Wasyria na mataifa jirani kujizuia kufanya matendo yatakayoteteresha usalama wa kanda ya Mashariki ya Kati.

Tamko lake limetolewa muda mfupi baada ya Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa kutoa tahadhari kwamba mzozo haujamalizika nchini mwake hata baada ya kuanguka utawala wa Assad.

Amesema bado mapigano yaendelea kaskazini mwa nchi hiyo kati ya makundi ya Wakurdi na yale yanayoungwa mkono na Uturuki.