1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern munich yatoka suluhu na Bayer Leverkusen 1:1

12 Aprili 2010

Finali ya FA ni kati ya Chelsea na Portsmouth

https://p.dw.com/p/Mucg
Kocha wa Schalke 04 F.Magath (kulia kabisa)Picha: dpa

MUHUTASARI:

Rais wa FIFA ,Sepp Blatter, anadai kuhakikishiwa kuwea, kuuwawa kwa EugeneTerre Blanche, hakutachafua mashindano ya Kombe lijalo la dunia nchini Afrika kusini.

China ,yaikabidhi Zimbabwe Uwanja mpya wa dimba, Na mabingwa wa Ethiopia, Saint George, wafunga nayo mkataba na kampuni la China kuijengea uwanja wa dimba.

Finali ya Kombe la FA nchini Uingereza, itakua kati ya Chelsea na Portsmouth, inayorudi daraja ya pili msimu ujao.

Katika Bundesliga ,Bayern Munich, yatoka suluhu bao 1:1 na Bayer Leverkusen, katika kinyan'ganyiro cha taji la Bundesliga.Taji mwishoe, litaenda wapi ?

BUNDESLIGA:

Kinyan'ganyiro cha taji la Bundesliga - mapambano 4 kabla msimu kumalizika kinaendelea kuwa mbio kati ya farasi 3 -Bayern Munich,Schalke na Bayer Leverkusen. Bayern Munich, ilimudu sare tu Jumamosi kati yake na Bayer Leverkusen baada ya kuachana bao 1:1. Hata hivyo, inadai iko njiani kutwaa mataji 3 msimu huu-Kombe la taifa la Ujerumani, Champions League -Kombe la klabu bingwa barani ulaya na la Bundesliga. Munich sasa inaongoza Ligi kwa pointi 2 na baada ya mpambano wa Jumamosi , stadi wao Schweinsteiger alisema:

"Kwa pointi 1 tulioondoka nayo hapa ,tunaweza kuridhika .Tunaoongoza sasa Ligi kwa pointi 2, huku yakiwa yamesalia mapambano 4 kumalizka msimu."Alisema Schweinsteiger.

Na Schalke, imekumbwa na msiba gani ?

Schlke ilikiona "kilichomtoa kanga manyoya ". Ilizabwa mabao 4:2, na Hannover na hata jogoo lao, Kevin Kuranyi, lilishindwa kuwika.

Kocha wa Schalke Felix Magath, alietaka kuitawaza schalke mabingwa msimu huu baada ya kuitawaza Wolfsburg,msimu uliopita mabingwa, aliungama kwamba Schalke haiviwezi vishindo vya kuvaa taji :

Masaa 24 baada ya mpambano huo, Magath aliungama aliposema, "Hatustahiki bado kuwa mabingwa ,kwani tumeregea mno."

Magath, akaongeza,

"Hakuna cha kulalamika.Hannover, ilistahiki ushindi wake.Tangu mwanzo wa mchezo hatukufanya mengi na hatukuonesha nia ya kutaka kushinda.Hivyo, tumeshindwa sasa mara ya pili mfululizo na hatuna budi bali kuridhia ukweli huo."Alisema Magath-kocha wa Schalke, iliosalia hatahivyo, nafasi ya 2 ya ngazi ya Ligi.

Stadi wa zamani wa Manu na Real Madrid, van Niestelrooy, aliwapatia Hamburg bado la ushindi pale ilipotoka nyuma na kuzoa pointi zote 3 kwa ushindi wa mabao 2:1 dhidi ya Bochum. Mpambano wapili jana, uliowaona mabingwa watetezi Wolfsburg,waliopigwa kumbo nje ya Euro-League na Fulham ya Uingereza, wakaitimua Nuremberg mabao 2:0. FC Cologne, imejikomboa kurudi daraja ya pili kwa kuzima jumamosi vishindo vya Hoffenheim na kurudi Cologne na mabao 2:0 .

KOMBE LA FA NA PREMIER LEAGUE:

Ama katika Premier League-ligi ya Uingereza, mwishoni mwa wiki ilikua pia zamu ya nusu-finali ya Kombe la FA. Baada ya firimbi ya miwsho ilifahamika kwamba, Chelsea, itacheza na Portsmouth inayorudi daraja ya pili msimu ujao kuamua wapi Kombe hilo la FA litaelekea ?

Portsmouth, jana iliizaba Tottenham mabao 2:0 baada ya kurefushwa mchezo.Chelsea, iliifedhehi Aston Villa, Jumamosi kwa mabao 3:0.

Katika kinyan'ganyiro cha taji la Premier League,ndoto ya Manchester united ya kutwaa taji hilo ili kufuta machozi kwa kutolewa nje ya champions league na Bayern Munich,ilianza kutoweka kwa kumudu suluhu tu ya 0:0 na Blackburn Rovers.Matokeo hayo yameiacha Manu pointi 1 nyuma ya Chelsea, inayoelekea kuvaa mataji yote 2 ya nyumbani.

Katika La Liga, Ligi ya Spain, Stadi wa dimba wa ulaya na dunia, Lionel Messi ameendelea kutamba: Kwa bao lake maridadi ,messi amehakikisha Barcelona inanyakua pointi zote 3 mfukoni mwa Real Madrid.

Bao jengine la Barca lilitiwa na Pedro.Mapambano 7 yakisalia, Barcelona,waliokwishakata tiketi ya nusu-finali ya Champions league, watumai kuondoka na taji la Spain na la ulaya msimu huu.

KOMBE LA DUNIA 2010

Kombe la dunia Afrika Kusini na China yakabidhi uwanja mpya wa dimba kwa Zimbabwe:Rais wa FIFA, Sepp Blatter amesema mwishoni mwa wiki kwamba, amehakikishiwa kuwa kuuwawa kwa Kionhozi wa wazungu wenye siasa kali za mrengo wa kulia, Eugene Terre' Blanche hivi majuzi, hakutaathiri vyovyote kombe lijalo la dunia litakaloanza juni 11. Blatter amekiambia kituo cha TV5-Europe kuwa hakutakua na ugomvi wa kikabila kwavile, serikali imeipa FIFA uhakikisho kwa njia isio ya moja kwa moja kupitia balozi wa Afrika kusini nchini Uswisi-makao makuu ya FIFA.

ZIMBABWE NA UWANJA MPYA

Na huko Zimbabwe,China iliojenga pia uwanja wa mpira mjini Dar-es-salaam uliofunguliwa rasmi mwaka uliopita, imeikabidhi Zimbabwe jana uwanja mpya baada ya matengenezo yaliogharimu dala milioni 10.

China iliijengea Zimbabwe uwanja wa mashabiki 60.000 hapo 1987,lakini ulifungwa kwa ajili ya matengenezo kwa miaka 3 iliopita.Sasa uwanja huo umegeuzwa kuwa wa kisasa kabisa.

Na huko Ethiopia, klabu bingwa St.George mwishoni mwa juma ilifunga mkataba na kampuni la majenzi la China kujenga nchini Ethiopia uwanja wa michezo. Makampuni ya china ni maarufu katika kujenga viwanja vya michezo barani Afrika.

Mwandishi:Ramadhan Ali/ RTRE

Mhariri: Miraji Othman