Bayern yarejea katika ushindi, Borussia yaangukia pua
16 Oktoba 2017Bayern Munich imerejea tena katika njia ya ushindi baada ya kubadilisha kocha wake Carlo Ancelotti wiki mbili zilizopita na kumpa kazi hiyo kocha wake mzoefu Jupp Heinckes , na kama alivyo daktari bingwa , aliweza kutambua matatizo yako wapi na kukipa makali ya wembe kikosi chake na kuinyoa Freiburg kwa mabao 5-0 katika mchezo wake wa kwanza kukaa katika benchi la ufundi . Heynckes alistaafu katikati ya mwaka 2013 baada ya kuipatia Bayern Munich mataji matatu katika msimu mmoja, Champions League, ubingwa wa ligi na kombe la Shirikisho DFB Pokal.
Mshambuliaji wa Bayern Munich na nahodha wa sasa wa timu hiyo Thomas Mueller amesema matokeo hayo yamewapa motisha zaidi ya kufanya vizuri zaidi.
"Tunapaswa kuendelea hivi hivi. Bila shaka tulicheza vizuri , lakini katika mchezo wa mpira , mchezo muhimu kila mara ni ule unaofuatia. Tumefanya kazi nzuri, tuliweza kubadilisha mchezo wetu kabisa, lakini pia kuna mambo fulani lazima tuyafanyie kazi. Bila shaka matokeo haya yanatupa nguvu zaidi na yatupasa kuendelea hivi hivi."
Bayern Munich imesogea hadi nafasi ya pili nyuma ya Borussia Dortmund ikiwa na pointi 17 , pointi 2 nyuma ya viongozi hao wa Bundesliga, ambao waliangukia pua siku ya Jumamosi katika mchezo maalum wa siku dhidi ya RB Leipzig. Katika jioni hiyo RB Leipzig ilivunja rekodi mbili za Dortmund , kutofungwa nyumbani katika Bundesliga kwa michezo 41, na pia timu hiyo inayoongozwa na kocha Ralph Hasenhuettl ilifikisha mwisho rekodi ya Dortmund ya kutofungwa msimu huu.
Borussia Dortmund hoi kwa RB
RB Leipzig iliishindilia Borussia Dortmund mabao 3-2 nyumbani, na kwa mara nyingine tena kuweka wazi ubovu wa safu ya ulinzi ya Borussia Dortmund, ambao umeonekana wazi katika michezo yake katika ligi ya mabingwa wa Ulaya Champions League , dhidi ya Totteham Hot Spurs na pia dhidi ya Real Madrid.
FC Kolon imebakia bila ushindi msimu huu na inakalia nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi , baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 nyumbani kwa VFB Stuttgart siku ya ufunguzi wa wiki ya nane ya bundesliga siku ya Ijumaa. FC Kolon bado ina pointi moja tu kibindoni na katika mchezo wa 9 FC Kolon ina miadi nyumbani na SV Werder Bremen , moja kati ya timu zilizoko majirani katika msimamo wa ligi, wakati Werder Bremen iko nafasi ya 17, FC Kolon iko nafasi ya 18.
Nani anaondoka na pointi tatu muhimu ni swali la kungoja na kuona. Kocha wa Bremen Alexander Nouri yuko katika mbinyo mkali wa kuleta mafanikio katika kikosi hicho, ama sivyo kibarua kitaota majani. Kinyume na mwenzake wa Kolon Peter Stoeger , anaungwa mkono kwa asilimia 100 na viongozi wa klabu pamoja na mashabiki.
Werder Bremen imetumbukia katika hali hiyo ngumu baada ya jana kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach, ambayo imepanda hadi katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.
Kocha Dieter Hecking wa Gladbach anasema.
"Ilikuwa ushindi usio na shaka, tulistahili kushinda kwa kiasi kikubwa. Tungeweza pia kupata bao ama mabao zaidi katika mchezo huo. Lakini jinsi gani na vipi timu iliweza kushinda kwa kweli ilikuwa vizuri sana."
Hamburg SV pia imo katika hali mbaya iliishia kushika nafasi ya 15 , baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Mainz 05 siku ya Jumamosi.
Bayer Leverkusen yaendelea kufanya vibaya
Mwanzo mbaya wa Bayern Leverkusen katika msimu huu wa ligi umendelea jana Jumapili , ambapo ilishindwa mara mbili kulinda ushindi wake dhidi ya Wolfsburg. Na Leverkusen ilijikuta ikikubali sare ya mabao 2-2 dhidi ya VFL Wolfsburg licha ya kwamba sare hiyo haijasaidia sana timu hizo ambazo ziko nafasi ya 12 na 14 zikitengana kwa pointi moja tu. Lakini hali hiyo haijamkosesha raha sana kocha mpya wa Wolfsburg Martin Schmidt ambaye anasema amefarijika kupata sare.
"Tumetoka uwanjani mara tano bila ya kufungwa, hii ina maana pia kwamba hatuachii mwanya hata kidogo. Hata tukiwa tuko nyuma tunapambana na kurudisha mabao. Hali hiyo ikiendelea kuwapo kichwani, na mafanikio ya pointi tatu pia yanafuatia."
Lakini kwa kocha wa Bayern 04 Leverkusen Heiko Herrlich haikuwa ni matokeo yanayoridhisha.
Heiko Herrlich (Bayer 04 Leverkusen)
"Leo tulitaka kushinda na iwapo tungetumia nafasi zilizopatikana tungetoka uwanjani tukiwa washindi. Lakini haikuwezekana na kwa kweli inakera."
Ushindi wa mabao 2-0 wa Schalke 04 dhidi ya Hertha BSC Berlin umeiweka timu hiyo katika nafasi ya 6 na Eintracht Frankfurt iliishinda Hannover 96 kwa mabao 2-1 na kuchupa hadi nafasi ya 7.
Na Ujerumani imeendelea kukalia nafasi ya juu ya orodha ya timu bora duniani kwa sasa iliyotolewa na shirikisho la kandanda duniani FIFA kama ilivyochapishwa leo Jumatatu na kuthibitisha timu za kiwango cha juu zitakazowekwa katika chungu kimoja katika upangaji wa timu zitakazoshiriki katika makundi ya fainali za kombe la dunia mwakani , pamoja na michuano ya mchujo ya kombe la mataifa ya bara la Ulaya.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman