Benki kufungwa Ugiriki kwa wiki nzima
29 Juni 2015Serikali ya Ugiriki imetoa tangazo rasmi kuwa benki zote nchini humo zitafungwa kuanzia leo hadi tarehe sita mwezi Julai, siku moja baada ya serikali kutangaza kutafanyika kura ya maoni kuamua suala hilo la mgogoro wa madeni unaoikumba nchi hiyo.
Raia wa Ugiriki wataruhusiwa kutoa euro sitini pekee kwa siku kutoka kwa mashine za benki za kutoa fedha lakini watalii wa kigeni ambao wanachangia pakubwa kwa uchumi wa nchi hiyo hawataathirika na agizo hilo.
Masoko ya hisa yaporomoka
Masoko ya hisa na ubadilishanaji wa fedha za kigeni yameporomoka sana hii leo kufuatia hatua hiyo ya Ugiriki. Masoko ya hisa ya Tokyo, Sydney, Shangahi na Hong Kong yameporomoka kwa zaidi ya asilimia mbili. Bei za mafuta na thamani ya sarafu ya euro pia zimeshuka.
Hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya Ugiriki inalenga kuulinda mfumo wa fedha nchini humo kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi miongoni mwa raia na wawekezaji ambao wamekuwa wakitoa kiwango kikubwa cha fedha katika kipindi cha siku kadhaa zilizopita na imezidi baada ya benki kuu ya Umoja wa Ulaya mwishoni mwa juma kusema haitaipa nchi hiyo mkopo wa kujikwamua.
Hali ya mashaka inayoikumba nchi hiyo ambayo heunda ikalazimika kuondoka kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro imesababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kupanga foleni ndefu katika benki kutoa fedha zao wakihofia athari zaidi za kiuchumi.
Kushindwa kwa Ugiriki na wakopeshaji wake wakuu Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha duniani IMF kufikia makubaliano muhimu ya kiuchumi mwishoni mwa juma kumemsababisha Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras kutangaza kutakuwa na kura ya maoni tarehe tano mwezi ujao kuhusu mgogoro huo ambao umedumu kwa miaka mitano sasa.
Matokeo yake wakopeshaji wamekasirishwa na kukataa kwa Ugiriki kuchukua mageuzi magumu ya kiuchumi na kukataa kuipa nchi hiyo mkopo zaidi wala kuirefushia muda wa kulipa madeni yake ambao muda wa mwisho wa kufanya hivyo ni hapo kesho. Ugiriki ilipaswa kuilipa IMF zaidi ya euro bilioni 1.5 ifikapo tarehe 30 mwezi huu.
Tsipras ahakikisha akiba ziko salama
Tsipras amewataka raia wa nchi yake kuwa watulivu na kuwahakikishia akiba zao zilizo katika benki ziko salama. Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker anatarajiwa kuitisha mkutano na wanahabari leo kujadili matukio hayo yanayojiri kuhusu Ugiriki.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya kiuchumi Pierre Moscovici amesema bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake na kuongeza kuwa Junker atatoa muongozo wa njia itakayofuatwa kufikia makubaliano hayo.
Mjini Berlin, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameitisha kikao cha dharura na viongozi wa kamati za bunge na viongozi wa vyama vya kisiasa huku Rais wa Ufaransa Francois Hollande naye akiongoza mkutano wa dharura na mawaziri wake mjini Paris.
Mwandishi:Caro Robi/afp/ap/reuters
Mhariri: Josephat Charo