1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia yachapisha ripoti ya rushwa

Christina Bergmann / Maja Dreyer6 Februari 2007

Rushwa na vitendo vya uhalifu ni matatizo ambayo pia Benki ya Dunia inakabiliana nayo. Miaka sita iliyopita shirika hilo linalosimamia mikopo na miradi ya maendeleo lilianzisha ofisi ya kupiga vita rushwa. Idara hiyo sasa imechapisha ripoti yake ya miaka miwili - 2005 na 2006.

https://p.dw.com/p/CHlf
Bwawa hilo nchini Lesotho ni mfano mmoja wa miradi ya Benki ya Dunia
Bwawa hilo nchini Lesotho ni mfano mmoja wa miradi ya Benki ya DuniaPicha: dpa - Bildfunk

Wafanyakazi 20 hadi 30 wa Benki ya Dunia kila siku wanachunguza kesi za rushwa katika miradi inayoendesha na shirika hilo. Mnamo miaka miwili iliyopita wamechunguza kesi 441. Makampuni 58 na watu 54 walitengwa kutoka kwenye miradi husika.

Kati ya makampuni hayo pia kuna kampuni moja la Kijerumani, kwani rushwa inatokea kila mahala, anasema David G. Hawkes, mmoja wa wachunguzi wa Benki ya Dunia: “Kuna aina tofauti za rushwa kwenye bara la Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Na kusema ukweli, kwa bahati nzuri au mbaya, sikuona kitu kipya barani Afrika ambacho sijawahi kukiona nchini Ujerumani.”

Kesi zinazochunguzwa zinajulikana hasa kupitia wafanyakazi wa Benki ya Dunia au wa mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kutoka nchi husika. Kwa hivyo ni vigumu kuzungumzia hali ya rushwa kwa jumla katika nchi fulani, kwa vile inawezekana kuwa jamii inaangalia vizuri na kuripoti kesi wanazoziona.

Katika kila tuhuma, wachunguzi wa Benki ya Dunia wanafanya utafiti wao huko huko wakisaidiwa na wataalamu. Ikiwa watagundua mambo yasiyo ya kawaida katika vitabu vya uhasibu watatoa ripoti kwa Benki ya Dunia ambayo huenda itaya toa makampuni au wafanyakazi husika kwa muda. Serikali ya nchi husika itafahamishwa na ikiwa ni lazima Benki ya Dunia itatoa ripoti kwa polisi. Ili kuzuia kesi hizo kutokea tena, Benki ya Dunia hujaribu kuweka wazi zaidi miradi yao.

Watu wanajua nini kinachotokea, anasema mchunguzi David Hawkes. Rushwa inafanyika wakati wote. Kwanza wafanyakazi wa nchi fulani, wanaosimamia mradi fulani, hupewa fedha au zawadi kama kompyuta au magari ili kujipatia maagizo. Bw. Hawkes amesema: “Halafu rushwa inafanyika katika kupasishwa mradi ambao hufanyika na idara za kiserikali. Wale wakaguzi wanakirimiwa chai na halafu rushwa inatumika kulipa bili.”

David Hawkes wa Benki ya Dunia hakubali rushwa hata kidogo. Ikiwa malipo ya chai yanaruhusiwa kiasi kidogo tu, mradi mzima utaathiriwa, kwa sababu kila mmoja anayeshughulishwa atajaribu kujipatia kipande chake. Mwisho fedha haitatosha kwa mradi wenyewe.

Gharama za uchunguzi huu wa rushwa unaofanyiwa na Benki ya Dunia ni zaidi ya Dola Millioni 10 kwa mwaka. Lakini shirika hili lina hakika kuwa fedha hizo zitaleta faida zaidi kuliko hasara.