Benki ya dunia yaonya kutokea mdororo wa uchumi duniani
18 Januari 2012Benki kuu ya dunia imesema kuwa mataifa ambayo yanatumia sarafu ya euro yanaonekana kuelekea katika mdororo wa uchumi. Tahadhari hiyo imekuja katika ripoti ya hali ya kiuchumi duniani , ambayo ilitolewa rasmi mjini Beijing leo Jumatano. Inatoa hali duni ya ukuaji ya asilimia 0.3 katika eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya euro katika mwaka 2012. Hali hiyo ni chini kutoka utabiri wa hapo kabla ya ukuaji wa asilimia 1.8. Ripoti hiyo inadokeza kuwa mzozo wa madeni ya kitaifa ndio sababu kuu ya utabiri ambao sio mzuri. Pia imeonya kuwa hali hiyo huenda ikasababisha kupungua kasi kwa ukuaji wa uchumi katika mataifa yanayoendelea, kama Brazil, India, Urusi na Afrika kusini. Hata hivyo , ripoti hiyo imesema kuwa ukuaji wa mataifa hayo unaweza kuendelea na kuyapita mataifa yaliyoendelea kiuchumi katika muda wa miezi 12 ijayo.